Jumatatu, Oktoba 27, 2014

AFA PAPO HAPO BAADA YA KUGONGWA NA GARI MBEYA

Mtembea kwa miguu aliyetambulika kwa jina la Atusungukile Mahenge (23) mkazi wa Uyole alifariki dunia papo hapo baada ya kugongwa na gari isiyofahamika iliyokuwa ikiendeshwa na dereva asiyefahamika jina wala makazi yake.
Tukio hilo limetokea jana majira ya saa 12:30 asubuhi huko Nane Nane darajani, kata ya Uyole, tarafa ya Iyunga, jiji na mkoa wa Mbeya. Chanzo cha ajali kinachunguzwa. Dereva alikimbia mara baada ya ajali na jitihada za kumtafuta zinaendelea. Mwili wa marehemu umehifadhiwa hospitali ya Rufaa Mbeya.
Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya Ahmed Msangi anatoa wito kwa madereva na watumiaji wengine wa vyombo vya moto kuwa makini wanapotumia vyombo hivyo ikiwa ni pamoja na kuzingatia sheria na alama za usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazoepukika. Aidha anatoa wito kwa yeyote mwenye taarifa za mahali alipo mtuhumiwa [dereva] kuzitoa katika mamlaka husika ili akamatwe na hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake.

0 comments:

Chapisha Maoni