Alhamisi, Septemba 11, 2014

TAREHE YA LEO KATIKA HISTORIA

Miaka 13 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 11 Septemba mwaka 2001, ndege mbili kati ya nne za abiria za Marekani zilizotekwa nyara ziligonga minara miwili pacha ya jengo la Biashara la Kimataifa la mjini New York huku ndege moja ikigonga jengo la Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) huko Washington. Ndege ya nne ililengwa ikiwa katika anga ya Pensylvania na kuanguka. Baadhi ya ghorofa za jengo la Biashara ya Kimataifa ziliporomoka na sehemu ya jengo la Pentagon pia ikaharibiwa katika mashambulizi hayo ya kigaidi. Karibu watu 3200 waliuawa katika mashambulizi hayo. Marekani ilitangaza kuwa mtandao wa al Qaida uliokuwa ukiongozwa na Usama bin Laden raia wa Saudi Arabia, ndio uliohusika na mashambulizi hayo. Baada ya matukio ya Septemba 11 nchini Marekani, kulianza wimbi la ubaguzi na mashambulizi dhidi ya Waislamu na matukufu ya dini yao katika nchi za Magharibi.
Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, Jenerali Agustino Pinoche kamanda wa wakati huo wa vikosi vya majini vya Chile aliipindua serikali halali ya Salvador Alande katika mapinduzi yaliyoungwa mkono na Marekani. Alande ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Kisoshalisti cha Chile, alichaguliwa kuwa Rais wa nchi hiyo mwaka 1970 na kuanza mara moja kutekeleza mpango wa kutaifisha mabenki, sekta ya madini na viwanda, suala ambalo lilikomesha maslahi haramu ya makampuni makubwa ya Kimarekani nchini Chile. Alande pia alikabiliana na ushawishi wa Washington nchini humo na kuifanya Marekani ianzishe vitimbi vya aina mbalimbali dhidi ya kiongozi huyo.
Miaka 66 iliyopita katika siku kama hii ya leo, aliaga dunia Muhammad Ali Jinnah, mwasisi wa Pakistan. Jinnah alizaliwa mwaka 1876 katika mji wa Karachi kusini mwa Pakistan. Muhammad Ali Jinnah alikuwa miongoni mwa shakhsiya walioasisi chama cha Muslim League mnamo mwaka 1906. Chama cha Muslim League awali kilikuwa kikijishughulisha na masuala ya kitamaduni na kidini, lakini baadaye kikaingia katika uwanja wa siasa na kutaka kuundwa nchi huru kwa ajili ya Waislamu wa India.

0 comments:

Chapisha Maoni