Jumatatu, Septemba 15, 2014

RUNGWE WASHINDWA KUTUMIA VIVUTIO VYAO VYA KITALII

WILAYA ya Rungwe mkoani Mbeya imeshindwa kupaa kiuchumi kwa kutovitangaza vivutio vya utalii vilivyopo. Kauli hiyo ilitolewa jana na Katibu Mkuu wa Christian and Gospel Ministry (CGM) wilayani humo, Watson Pamesa wakati wa makabidhiano ya jengo la kufungia mitambo kwa ajili ya Redio Rungwe inayotarajia kufunguliwa hivi karibuni.
Makabidhiano ya jengo la ghorofa moja yalifanyika jana baada ya uongozi wa Christian kukutana na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Veronica Kessy ambapo mapendekezo na muhtasari wa kikao hicho yalipelekwa katika kikao cha Baraza la Madiwani Agosti 26 mwaka huu kujadiliwa.
Pamesa alisema waliiandikia halmashauri hiyo barua yenye kumbukumbu namba RDC/E.1/117/97 ya Agosti 7, 2013 ambapo ilijibiwa Mei 30, 2014 kwa barua yenye kumbukumbu namba TKY/7.6/VOL.010/2014 iliyosainiwa na Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Elias Sangi kwamba ombi lao limekubaliwa.
Alisema wilaya za Kyela na Ileje zimetokana na Rungwe iliyoanzishwa mwaka 1900 wakati wa ukoloni hivyo kuwa na vivutio vya kihistoria ambavyo ni Vinyonga na Nyani wekundu wanaoishi mlima Rungwe, daraja la Mungu, Ziwa ngozi na kisima ambacho maji yake hayakauki, mti Rungwe uliozaa jina la wilaya hiyo na unatibu magonjwa zaidi ya 45.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Christian and Gospel Ministry wilayani humo Amoni Mwakilomo mbali na kuipongeza halmashauri ya wilaya hiyo kwa kuwaunga mkono pia amesema mchakato wa redio umefikia ukingoni na sasa wanajipanga kuanzisha gazeti kwa lengo la kutoa huduma ya kihabari kwa wanarungwe.
Chrispin Meela mkuu wa wilaya hiyo alisema watakuwa bega kwa bega na mtandao huo ili kuhakikisha wilaya hiyo inatumia Digital na kuondokana na analojia kwa kuuhabarisha umma kwa matukio mbalimbali na kukuza pato la ndani nje wilayani humo.

0 comments:

Chapisha Maoni