Wananchi wa jiji la Mbeya na maeneo jirani ambao wanaitumia barabara kuu ya kutoka na kuingia mjini hapa kupitia mji mdogo wa Uyole eneo la Makasini wamekumbwa na adha kubwa ya usafiri baada ya madereva wa malori kuegesha barabarani magari yao na kufunga barabara hiyo.
Chanzo cha tukio hilo linalokwamisha safari za watu na shughuli nyingine za kiuchumi zinazotegemea usafiri wa nchi kavu mkoani Mbeya ni kitendo cha askari wa barabarani kukamata malori yaliyopaki pembezoni mwa barabara, kung'oa namba za usajili za malori hayo, kutoza faini na kisha kutoa stakabadhi bandia.
Madereva na matingo wa malori hayo kwa nyakati tofauti wameiambia Fichuo Tz kuwa kitendo walichofanyiwa si cha kistaarabu na ni kinyume cha kazi yao kwakuwa wamekuwa na mazoea ya kutoza tozo kinyume na utaratibu unaotakiwa kwa kutoa risiti bandia. Mpaka timu ya Fichuo inaondoka katika eneo hilo la tukio tayari msururu wa magari ulikuwa umekwisha kuwa mrefu kwani ni magari mengi yatokayo nchi za Congo DRC, Zambia, Kenya, Msumbiji na nchi nyinginezo hufanya safari zake kupitia barabara hiyo mkoani hapa.
Wanachokitaka wao hasa ni kukutana na mkuu wa mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro pamoja na mbunge wa Mbeya mjini, mh. Joseph Mbilinyi ambao wote hawapo mkoani Mbeya.
Baadhi ya picha za tukio ziko hapa:
0 comments:
Chapisha Maoni