Jeshi la Polisi limefanikiwa kumkamata Ali Suleiman Rashid (34)
akiwa na mikoba 14 ya wanawake aliyohifadhia dawa za kulevya zenye uzito
wa kilo tano akitokea Oman katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid
Amani Karume visiwani humo.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Makao
Mkuu ya Polisi Ziwani mjini Zanzibar, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na
Makosa ya Jinai (DCI ), Yussuf Ilembo alisema kuwa mtuhumiwa huyo raia
wa Tanzania amekamatwa muda mfupi baada ya kushuka kutoka Ndege ya Oman
yenye namba za usajili .WY.717 iliyokuwa ikitokea Muscat.
Ilembo alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa Julai 9,
saa 8 mchana akiwa amehifadhi mikoba hiyo katika sanduku kubwa lenye
rangi nyeusi na maofisa wa upelelezi waligundua ndani yake kuwemo mikoba
14 iliyokuwa na dawa hizo ikiwa imeshonewa kwa vitu maalumu.
Dawa hizo za kulevya zina uzito wa kilo 5.605, zilihifadhiwa kwenye mikoba 14 inayotumiwa na wanawake. Upelelezi kukamilika, atafikishwa mahakamani mara moja.alisema DCI Ilembo.
Alisema polisi inaendelea na uchunguzi wake ili
kusaka mtandao wa watu wanaojishughulisha na vitendo hivyo kwa
kuchunguza njia mbalimbali za mawasiliano za mtuhumiwa huyo
aliyekamatwa.
Kwa mujibu wa polisi, mtuhumiwa huyo alikuwa
akitumia hati ya kusafiria namba AB 363906 iliotolewa Desemba 29 mwaka
2009 Makao Makuu ya Idara ya Uhamiaji Dar es Salaam na tayari
ameshasafiri katika nchi za Brazil, China, Japan, Hong Kong, Afrika
Kusini na Falme za Kiarabu.
Ilembo aliwataka wananchi kuchukua hatua kwa
kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kuwafichua kwa siri, wanaoingiza
dawa za kulevya na wauzaji ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Wakati wa kulindana, kuleana na kuoneana aibu umekwisha, kila mmoja ajione ana wajibu wa kulilinda taifa kwa maisha yake na vizazi vijavyo.alisema DCI Ilembo.
Mapema mwaka huu polisi walikamata mabegi mawili
yakiwa na dawa za kuelvya katika chumba cha kuondokea abiria, Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume.




0 comments:
Chapisha Maoni