Wakati Serikali ikiendelea kutafuta ‘mwarobaini’ wa kushuka kwa
elimu, wadau mbalimbali wameitaka kuachana na mpango wa kupanga bei
elekezi kwenye ada za shule na vyuo nchini kwa kuwa hilo siyo suluhisho.
Wakizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti
iliyochunguza hali ya sheria na sera za ushindani wa kibiashara nchini,
washiriki hao walisema baadhi ya viongozi wakiwamo wabunge wamekuwa
wakipendekeza shule na vyuo vyote nchini kutoza viwango sawa vya ada,
bila kuzingatia tofauti za kipato kwa wananchi.
Akizungumza katika mkutano uliofanyika hivi
karibuni jijini hapa, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa
Kupunguza Umaskini (REPOA), Profesa Samuel Wangwe alisema elimu haipaswi
kuwekewa kikomo cha ada, badala yake zitafutwe sababu zilizoshusha
hadhi ya taasisi hiyo.
Elimu siyo bidhaa unayoweza kuipangia bei, kama mtu anaweza kumlipia mtoto ada Sh4 milioni alipe, kwa sababu wapo watu wanaowalipa watoto wao ada Ulaya Sh20 milioni.alisema Wangwe.
Alisema shule za sekondari za umma ikiwamo Pugu
zilikuwa zikitegemewa kwa kufaulisha wanafunzi, lakini hivi karibuni
zimekuwa zikifanya vibaya kitaaluma. Hivyo ni vyema serikali ikatafuta
sababu za matokeo mabaya, badala ya kushughulikia viwango vya ada pekee
yake.
Kama shule za umma zinafanya vizuri hata hao wanaoweka ada ya Sh4 milioni watapunguza tu.aliongeza.
Mwakilishi kutoka Tume ya Ushindani (FCC),
Shadrack Nkelebe, alisema wadau wa elimu wanapaswa kuwekewa mazingira
mazuri ya ushindani yatakayowawezesha kuboresha taasisi hiyo na
kuwanufaisha walaji kwa kuongeza ubora wa elimu.
Alisema hivi sasa dunia inaondokana na upangaji wa
bei katika biashara ili kuwaongezea wafanyabiashara uwanja wa
kushindana kwa uhuru na kwa kufuata sheria.
Udhibiti wa shule unaweza kupunguza ubora wa elimu, acha kupunguza ada kwa matajiri na kuongeza kwa maskini.alisema Nkelebe.
Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo uliofanyika
Dar es Salaam pekee, Dk Halima Noor kutoka REPOA, alisema ripoti hiyo
imebaini mambo kadhaa yanayowakera wananchi, ingawa asilimia 52 ya watu
waliohojiwa walisema hawaijui taasisi yoyote inayoshughulikia ushindani
wa kibiashara nchini.
Ripoti hiyo imebaini kuwa wananchi wanaamini
kwamba baadhi ya kampuni zinapanga bei ya bidhaa zake kwa lengo la
‘kuwaumiza’ wateja, jambo lililo kinyume na sheria ya ushindani katika
biashara.
Asilimia 48 walisema kampuni zinapanga bei za bidhaa kinyume cha sheria, wengine walisema ingawa sekta ya usafiri Dar es Salaam ina ushindani mkubwa, gharama ya nauli ipo juu.alisema Dk Halima.




0 comments:
Chapisha Maoni