Alhamisi, Julai 17, 2014

LORI LAINGIA KILABUNI NA KUUA WATANO IRINGA

Watu 5 wamekufa papo hapo wakiwemo watu watatu wa familia moja na wengine 3 kujeruhiwa vibaya baada ya lori la kubebea mizingo kuparamia nyumba ya kuuzia pombe katika kijiji cha Ugwachana, Manispaa ya Iringa.
Akizungumza na FICHUO leo Alhamisi Julai 17, 2014, Kamanda wa polisi mkoani humo, Ramadhani Mungi, amesema ajali hiyo imetokea jana saa tatu usiku katika kijiji hicho na Kitongoji cha Isimila katika Wilaya ya Iringa katika barabara Kuu ya kutoka Iringa kwenda Mbeya.
Amesema ajali hiyo imehusisha lori lenye namba T 878 AFB likiwa na trela lililokuwa lenye namba T 570 AYY mali ya Kampuni ya MT Huwei ya mkoani humo, lililokuwa linaendeshwa na Juma Omary (40), mkazi wa Makorongoni na kuwa liliacha barabara na kuparamia Kilabu cha kunywea pombe ya kienyeji na kuua watu hao wakiwa ndani ya kilabu hicho.
Amewataja marehemu kuwa ni Leonard Mkendela (35), Neema Mkendela, na Kamsia Mkendela, (wote wa familai moja) na wengine wawili ambao ni Mke na Mume, Ester Mwalomo na Oscar Zosama (25) wote wakazi wa eneo hilo.
Hata hivyo, amesema majeruhi wa ajali hiyo ni pamoja na dereva wa gari hilo, Juma Omary (40), Musa Kadege (25), mkazi wa kijiweni, na Kasimu Mambo (44) mkazi wa Kijiweni mkoani.
Amesema majeruhi hao wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Iringa, na kuwa afya za watu wawili kati yao wakiendelea vizuri na kuwa dereva wa gari hilo hali yake ni mbaya ambapo amelazwa katika wodi ya wagonjwa mahututi (ICU).

0 comments:

Chapisha Maoni