Jumatatu, Julai 21, 2014

SUMAYE KUZINDUA ALBUM YA ROSE MUHANDO

WAZIRI Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi wakati wa uzinduzi wa albamu ya mwimbaji mahiri wa Injili nchini, Rose Muhando iitwayo Kamata Pindo la Yesu.
Uzinduzi huo unatarajiwa kufanyika Ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam, Agosti 3, mwaka huu, ambapo waimbaji mbalimbali wa muziki wa kiroho watatumbuiza siku hiyo.
Baadhi ya waimbaji mahiri ambao hadi sasa wameshathibitisha kushiriki uzinduzi huo ni Upendo Nkone, John Lissu, Bonny Mwaitege na Ephraim Sekeleti.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotions, ambao ni wadhamini na waratibu wa uzinduzi huo, Alex Msama, il isema maandalizi muhimu kuhusu uzinduzi huo yanaenda vizuri.
Tumekubaliana tumuombe Waziri Mkuu mstaafu Sumaye aje atupe baraka kwenye uzinduzi huo, nafurahi kusema ni mtu wa watu, amekubali kujumuika na wadau wengine siku hiyo. Hili ni jambo la furaha kubwa kwetu. Wasanii mbalimbali tunaendelea kuzungumza nao kuhakikisha wanashiriki katika uzinduzi huo, ambao utakuwa moto wa kuotea mbali
alisema Msama katika taarifa yake.
Sumaye alikuwa Waziri Mkuu katika Serikali ya Awamu ya Tatu kuanzia mwaka 1995 hadi mwaka 2005, akiwa ndiye Waziri Mkuu aliyekaa muda mrefu katika wadhifa huo kwa historia ya Tanzania.

0 comments:

Chapisha Maoni