Jumapili, Julai 20, 2014

SIRI YA MAFANIKIO YA SHULE YA IGOWOLE BAADA YA KUWA YA KWANZA KITAIFA

Uwepo wa nidhamu ya wanafunzi, ushirikiano wa walimu pamoja na wazazi umesaidia shule ya sekondari ya Igowole, wilayani Mufindi Mkoani Iringa kushika nafasi ya kwanza kitaifa katika matokeo ya kidato cha sita mwaka huu.
Mkuu wa shule ya Sekondari Igowole ambaye pia ni mwenyekiti wa wakuu wa Shule za Sekondari Mkoani Iringa Bw. Andrew Kauta amesema shule yake imekuwa inajitahidi katika kuwa na ufaulu mzuri kitaifa kwa kila mwaka ambapo mwa 2011 ilikuwa nafasi ya 46,2012 nafasi ya 13,2013 nafasi ya 8 na mwaka huu wamekuwa nafasi ya kwanza.
Bw:Kauta ameongeza kuwa licha ya kushika nafasi hiyo shule yake inakabiliwa na changamoto ya kutowepo kwa miundo mbinu ya maji ya bomba,ukumbi wa chakula,madarasa,maabara,mabweni hali iliyopelekea nyumba yake kutumiwa na baadhi ya wanafunzi kwa malazi na jumla ya walimu waliopo shuleni hapo ni 37 ingawa hitaji lake ni walimu 60.
Aidha amesema wana mpango wa mda mrefu wa kuthibiti wanafunzi katika utumiaji wa mitandao ya kijamii na vitabu ambavyo havijathibitishwa na mamlaka husika,uwepo wa mitihani ya ujilani mwema na walimu kujiendeleza kimasomo,kusoma vitabu mbalimbali na kushirikishana katika maandalio ya masomo.
Kwa upande wa mwalimu wa nidhamu Bw.Kisyaka Chotoda amesema wamekuwa na vikao vya mara kwa mara kati ya walimu wakishilikiana na kamati ya shule pamoja na wanafunzi pia kuwafanyia uchunguzi wa kidaktari kwa ajili ya utambuzi wa mambo ya magonjwa na mimba.
Hata hivyo shule ya Igowole ilianzishwa mwaka 1988 ikimilikiwa na wazazi ambapo mwaka 2003 ilisajiliwa na kumilikiwa na selikali ikiwa na kidato cha kwanza cha nne na mwaka 2008 ulianzishwa mpango wa elimu ya juu kwa wasichana kwa michepuo ya HKL,HGK,HGL NA EGM.

0 comments:

Chapisha Maoni