Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kwa mara nyingine ametunukiwa tuzo la kimataifa.
Zamu hii kwa kuwa mshindi wa Tuzo la Nyota wa Demokrasia Afrika 2014 – Icon of Democracy Award Winner for 2014 in Africa.
Kwa mujibu wa barua aliyoandikiwa Rais Kikwete na kupokelewa Ikulu,
Dar Es Salaam, Rais Kikwete amekuwa mshindi wa kwanza, na kwa mbali
kabisa katika mchuano na marais watatu wa Afrika ambao walifikia
mwishoni mwa mchuano wa kuwania tuzo hilo.
Katika barua hiyo, Mchapishaji na Mhariri Mkuu wa Jarida hilo, Pastor
Elvis Iruh akizungumza kwa niaba ya Kamati ya Tuzo 2014, amesema kuwa
uongozi wa Rais Kikwete umekuwa ni hadithi ya kusifiwa ya mafanikio
katika Bara ambako hadithi za namna hiyo siyo nyingi.
Tuzo hiyo hutolewa na Jarida la The Voice
na mwaka jana mshindi alikuwa ni Rais Bai Koroma wa Sierra Leone ambaye
alikuwa ni mshindi wa pili wa Tuzo hiyo ambayo ilitolewa kwa mara ya
kwanza kwa Rais wa Kwanza wa Zambia, Mzee Kenneth Kaunda.
Sherehe maalum ya kukabidhi tuzo hiyo imepangwa kufanyika Oktoba 17,
mwaka huu, 2014, katika Hoteli ya Van der Valk, iliyoko Almere,
Uholanzi.
Miongoni mwa sifa nyingine, Rais Kikwete anatunukiwa Tuzo hiyo kwa
sababu ya kuwa msimamizi mzuri na wa kweli wa demokrasia, kuendelea
kuhakikisha kuwa amani, utulivu na maendeleo vinaendelea kupatikana
katika eneo la Afrika ambalo limepitia vipindi vingi vya migogoro na
matatizo.
Aidha, gazeti hilo linasema kuwa Rais Kikwete amekuwa kiongozi wa
mfano, kimataifa na kikanda, na linatoa mfano wa mchango wake katika
kusuluhisha mgogoro mkubwa wa kisiasa nchini Kenya kufuatia uchaguzi
mkuu wa 2007.
Rais Kikwete pia anasifiwa kwa mchango wake katika kusimamia
maendeleo ya Tanzania katika nyanja mbali mbali – kilimo, elimu,
miundombinu, maendeleo ya viwanda, utalii na pia mchango wake katika
kuendeleza vijana na kutoa nafasi nyingi kwa akinamama kushika nafasi
nyingi za uongozi.
Jarida la The Voice pia limempongeza Rais
Kikwete kwa kuimarisha Umoja na Muungano wa Tanzania na kutoa nafasi kwa
wananchi kujadili na kukubaliana kuhusu Katiba mpya ya Tanzania.
Aprili mwaka huu, Rais Kikwete alitunukiwa tuzo la kuwa kiongozi
mwenye mchango mkubwa zaidi katika maendeleo ya Afrika kwa mwaka 2013 – The Most Impactful Leader in Africa 2013.
0 comments:
Chapisha Maoni