Jumanne, Julai 01, 2014

MAXIMO: MARUFUKU KUMPELEKA ANDREY COUNTINHO DISCO

KOCHA Mkuu wa Yanga,  Marcio Maximo ‘The  Chosen One’ amewaambia wachezaji wa timu hiyo wafanye kila kitu na kiungo Mbrazil,Andrey Coutinho lakini ni marufuku kumpeleka disko au Bongofleva.
Bosi huyo ambaye ni chaguo la uongozi na mashabiki wa Yanga aliyepewa jina maarufu la The Chosen One wakimaanisha ni mteule, alikutana rasmi na wachezaji wake jana Jumatatu makao makuu ya Yanga pale Jangwani, Dar es Salaam.
Maximo ambaye anayafahamu vizuri mazingira ya Kiafrika hususani Tanzania, amewataka wachezaji hao kumfundisha Coutinho mambo mazuri badala kumwonyesha mambo ya starehe ambayo yanaweza kuathiri nidhamu yake ya mazoezi.
Akizungumza kwa uchangamfu huku wachezaji wakiwa na umakini mkubwa, aliwataka kutomhofia mchezaji huyo na badala yake wamchukulie kama mtu wa kawaida washirikiane nae kwa kila jambo pamoja na kumwelekeza jinsi mambo yanavyokuwa na yeye atatekeleza kwa vile ni msikivu na muwajibikaji.
Wachezaji kadhaa wa kigeni wamekuwa wakipepesuka kiutendaji wanapotua kwenye klabu za Simba na Yanga kutokana na kusifiwa kupitiliza na mashabiki ambao huwapeleka kwenye mambo ya starehe. Wachezaji wengi wenye asili ya Jamhuri ya Kidemorasia ya Congo, Rwanda na Kenya ndio waliowahi kukumbwa na tatizo hilo la kuendekeza starehe na wengine kuishia kupoteza nafasi zao na kufukuzwa baada ya muda.

0 comments:

Chapisha Maoni