Uongozi wa klabu ya Yanga umetoa ruksa kwa klabu ya Free State
Stars ya Afrika Kusini kufanya mazungumzo kama wanataka kumsajili
mchezaji wao nyota, Mrisho Ngasa.
Awali klabu hiyo ilishangazwa na hatua ya klabu
hiyo kubwa inayoshiriki Ligi Kuu Afrika Kusini kumchukua mchezaji wao
kinyemela na kumfanyisha majaribio kinyume na taratibu na kanuni za
mpira wa miguu duniani.
Ngassa alikwenda kufanya majaribio na timu hiyo ya
Afrika Kusini takribani wiki mbili zilizopita, na uongozi wa timu hiyo
ulikuwa tayari kutoa Sh132 milioni ili kumsajili mchezaji huyo.
Hata hivyo, mpango huo uligonga mwamba kutokana na
ukweli kuwa viongozi wa Free State Stars walifanya mpango huo na Ngassa
kinyemela.
Hatua hiyo iliufanya uongozi wa Yanga kulishutumu
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kuhusika moja ka moja na mpango
huo kwani haukuridhishwa na jinsi Ngassa alivyoondoka nchini kwenda
Afrika Kusini wakati alikuwa kwenye Kambi ya Taifa Stars.
Katibu Mkuu wa Yanga, Benno Njovu alisema kuwa
wametoa fursa kwa uongozi wa timu hiyo ya Afrika Kusini kuja nchini na
kufanya mazungumzo mezani ili kufanikisha suala hilo.
Njovu alisema kuwa Yanga haina haja ya kumzuia Ngassa kwenda kucheza soka lake Afrika Kusini kwani hiyo ndiyo kazi yake.
0 comments:
Chapisha Maoni