TIMU ngeni katika Ligi Kuu ya msimu ujao ambao utaanza Septemba 20,
ni Ndanda FC ya Mtwara, Polisi ya Morogoro na Stand United ya Shinyanga
zikiziba nafasi ya zilizoshuka ambazo ni Ashanti Utd, JKT Iljoro na
Rhino ya Tabora.
Wakati timu zote zikijianda kwa ligi hiyo, timu ngeni zinapaswa kuiga
ari ya timu ya Mbeya City iliyoingia Ligi Kuu kwa mara ya kwanza msimu
uliopita na kutwaa nafasi ya tatu, ikitanguliwa.
Kama timu ya Mbeya City imeweza kuzichachafya timu kongwe na kuwa
tishio, kwa nini timu za Ndanda FC, Stand United na Polisi ya Morogoro
zisiweze? Timu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom hakuna yenye hakimiliki
ya kutwaa ubingwa mara zote kwani mashindano ni tendo la kupimana uwezo
katika jambo. Ni makabiliano yenye lengo la kuwania jambo baina ya
pande mbili au zaidi. Mwenye bidii ndiye anayeibuka mshindi.
Timu hizo zisiogope majina yaliyozoeleka ya wachezaji kwani wote wana
miguu miwili na kuingiza wachezaji 11 uwanjani kama wao. Kadhalika
wasihofie umaarufu wa vilabu kwani navyo pia vilianza kama vyao. Madhali
wamejumuishwa na timu kongwe zenye uzoefu, nazo zijione kuwa sawa kwani
zimewekwa pamoja kuwania ubingwa utakaopatikana kwa ushindi dhidi ya
zingine. Katika michezo kuna waamuzi wanaosimamia haki.
Nazikumbusha kungali mapema kuwa “mwenye kisu kikali ndiye alaye
nyama. Anayekishika kisu kikali ndiye anayeweza kuikata nyama vizuri.
Methali hii yatukumbusha kuwa aliyejiandaa vizuri ndiye awezaye
kufanikiwa katika jambo fulani. Nawashauri wajiandae ipasavyo kabla ya
kuliingilia jambo. Kwa kuwa Ligi Kuu iliyokuwa ianze Agosti 28 mwaka huu
imesogezwa mpaka Septemba 20 kupisha michuano ya Klabu Bingwa ya Afrika
Mashariki na Kati itakayoanza Agosti 8 na kumalizika Agosti 24 nchini
Rwanda, ni kama nafuu ya mchukuzi kwa timu hizo kuwa na muda zaidi wa
kujiandaa.
0 comments:
Chapisha Maoni