TUKIO la ujambazi ambalo liliua watu
watatu wanaosadikiwa kuwa majambazi, limechukua sura mpya baada ya
silaha waliyokuwa wakitumia majambazi hao kugundulika kuwa ilikuwa
ikimilikiwa na askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), Sospeter
Peter Manyika ambaye kwa sasa yuko rumande.
Kukamatwa kwa Manyika kumethibitishwa na
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas lakini hakuwa
tayari kusema chochote juu ya kuwekwa rumande kwa askari huyo.
Ni kweli tulimkamata (Manyika) baada ya kufanya uchunguzi na kugundua kuwa silaha waliyokutwa nayo majambazi ni mali yake
alisema bila ya kufafanua chochote.
Vyanzo vya habari kutoka ndani ya jeshi
la polisi vilisema kuwa Manyika alikamatwa Julai 9 mwaka huu akiwa
kazini Ngorongoro, baada ya kubainika kuwa silaha hiyo ilikuwa mali
yake.
Habari ziliendelea kusema kuwa Manyika
ambaye ni dereva wa gari kubwa la FFU anamiliki silaha aina ya shotgun
namba A 947514 M – Pump Action iliyotengenezwa Marekani.
Siku ya tukio la kuuawa kwa majambazi
hao watatu ambao walikuwa wakitumia gari aina ya Toyota Corolla lenye
namba za usajili T 762 CWE, walikuwa wanakwenda kupora fedha katika
kampuni ya Arusha Ceramic Centre inayojishughulisha na utengenezaji wa
vigae.
Majambazi hao waliuawa Julai 4 mwaka huu
saa 10:20 jioni jirani na Kiwanda cha Bia (TBL) eneo la Njiro Jijini
Arusha na silaha hiyo ilikuwa na risasi tatu.
Majambazi hao walitambuliwa kwa majina
ya Selemani Walii(25) mkazi wa Kaloleni Jijini Arusha, Walter John (30)
na mdogo wake Fred John (21) wote wakazi wa Sekei wilayani Arumeru
mkoani Arusha.




0 comments:
Chapisha Maoni