Jumatano, Julai 30, 2014

BARUA KWA MO-MUSIC

Mo Music. Bila shaka u mzima wa afya na unaendelea na majukumu yako ya kila siku vyema. Kama ndivyo, kwangu ni furaha. Miye nipo sawa naendelea na mchakamchaka wa kusaka mkate wa kila siku.
Kwa mara ya kwanza ninakuandikia barua, eneo ambalo huwa nalitumia kuwasiliana na wasanii mbalimbali wa Tanzania na watu maarufu kwenye jamii. Lengo ni kuwekana sawa ili sanaa yetu iendelee kupaa.
Kabla sijaenda mbali zaidi, nataka kukuhakikishia kuwa kipaji cha muziki unacho, tena cha hali ya juu sana. Nikikutazama nayaona mafanikio makubwa sana mbele yako. Ni subira tu. Zaidi ya kuvuta subira ni juhudi katika kazi.
Ikiwa utaongeza juhudi na kuwa makini na jamii ambayo ndiyo wateja wako, bila shaka utatoboa Kimataifa. Lazima usome soko, ujue jamii inataka nini kutoka kwako, ndipo ulipuke! Ngoma yako ya Basi Nenda kiukweli ni nzuri, mashairi yamepangiliwa vizuri, umeimba vizuri na hata studio nao wameitendea haki.
Kitu ambacho nimejiuliza sana, ni kwamba lengo lako la kuachia Basi Nenda ilikuwa ni kutesti gemu, kutoka au kufanikiwa kimuziki?Nimekuuliza hivyo kwa sababu naona baada ya kuachia ngoma hiyo, umekaa kimya jumla. Kwanza fahamu kuwa asilimia kubwa ya wasanii wanaotoa nyimbo zao kwa mara ya kwanza huwa hazikubaliki haraka.
Imezoeleka msanii anaachia ya kwanza, anasikilizia kisha anatoa na nyingine na nyingine, wakati mwingine mpaka msanii afikishe vibao vitatu au vinne ndipo anapokubalika na anakuwa ametoka kimuziki.
Kwa upande wako (na wasanii wengine wachache sana) imekuwa tofauti. Umetoa wimbo mmoja tu, jamii imeuelewa. Kwa maneno rahisi ni kwamba umeshatoka kimuziki. Kama kutoka umeshatoka, je, unafanyaje sasa ili uweze kuendelea kung’aa katika soko hili la ushindani?
Kwa ninavyojua muziki wetu wa Kibongo ambao naweza kusema wasanii wenyewe mmeumaliza, wimbo hauwezi kukaa muda mrefu kabla ya kuchuja, hii inamaana kuwa, kama utatulia kwa muda mrefu, Basi Nenda unaweza ukaenda na wewe ukapotea jumla!
Je, ndiyo lilikuwa kusudio lako? Muziki ni ushindani, nakuhakikishia kama hutaamka na kuchomoka na kitu kingine fasta, unaweza kupotezwa.
Zinduka, fanya mambo. Lakini jambo la msingi ambalo nakushauri hakikisha pini inayofuata iwe mfuniko wa nguvu kuliko Basi Nenda, maana kibao hicho kimeshika vibaya mno, sasa kama ukija na wimbo wa kawaida, unaweza usisikike ikawa umejiharibia.
Ongeza ubunifu, anzia pale ulipoishia kwenye Basi Nenda, kisha nenda hatua nyingi zaidi mbele ili uzidi kufunika kwenye gemu.Namalizia kwa kusisitiza kuwa kama kutoka umeshatoka Mo, sasa anza mashambulizi ili ukae kileleni kwenye muziki wa Bongo Fleva.
Asitokee mtu wa kukudanganya kuwa huwezi, bado chipukizi na maneno mengine ya kuvunja moyo. Chukua haya kutoka kwangu, unaweza! Ni suala la kuamua tu na kuonyesha vitendo.
Yuleyule,
Mkweli daima

0 comments:

Chapisha Maoni