Sista wa kanisa katoliki jimbo la Mtwara sista Sophia Nampwapwa
amefariki dunia kwenye ajali mbaya ya barabarani, baada ya gari
alilokisafiria kuacha njia na kupinduka mara 2 kwenye barabara ya chuno
katika manispaa ya Mtwara/Mikindani.
Sista Sophia amefariki muda mfupi baada ya kufikishwa hospitali ya
rufaa ya mkoa wa Mtwara ya Ligula, na miongoni mwa viongozi waliostushwa
na ajali hiyo na kufika hospitalini hapo kufuatilia, ni askofu wa jimbo
la Mtwara Gabriel Mmole.
Kamanda wa polisi mkoa Mtwara kamishna msaidizi mwandamizi wa
polisi Augustine Ollomi amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo majira ya
saa 11 jioni, ikihusisha gari aina ya land rover lenye usajili namba T
589 AAG na kuongeza, polisi inamshikilia dreva wa gari hilo
aliyetambulika kuwa Godwin, kwa uchunguzi zaidi.
Hata hivyo baadhi ya walioshuhudia ajali hiyo wamesema, imetokea
wakati dreva alipokuwa akijaribu kumkwepa mpanda baskeli aliyekatisha
ghafla barabarani huku dreva huyo akidaiwa, alikuwa kwenye mwendo kasi.
Akizungumzia kifo cha sista Sophia Nampwapwa kaimu mama mkuu
shirika la masista wa mkombozi Mtwara sista Veronica amesema, wamepokea
kwa mstuko mkubwa kifo hicho lakini wanawashukuru wote waliojaribu
kuokoa maisha yake ikiwa ni pamoja waliombeba na kumwaisha hospitalini
pamoja na madaktari.
0 comments:
Chapisha Maoni