Kwa mara nyingine serikali kupitia viongozi na watendaji wake akiwamo
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), wamedai kwamba kiasi cha Dola za
Marekani milioni 250 zilizopaswa kuendelea kuwapo katika ‘Tegeta Escrow
Account’ si mali ya serikali na hivyo si mali ya umma. Akaunti hiyo
ilifunguliwa na serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la
Umeme Tanzania (Tanesco) pamoja na kampuni ya Independent Power Limited
(IPTL).
Kwa bahati mbaya sana viongozi wa serikali wamekuwa
wakiendelea kurudia kuueneza huo uongo kwamba fedha hizo si mali ya
umma. Inasikitisha pia kwamba vyombo vya habari vimekuwa navyo vikibeba
na kusambaza huo uongo bila kuhoji na kuchunguza. Inashangaza sana pia
asasi za kiraia nazo zimekaa kimya. Inatisha na kushangaa tena kuona
wapinzani wakimwachia suala hili Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi),
David Kafulila, pekee wakati mapambano dhidi ya rushwa ni ajenda kuu ya
wapinzani. Kafulila amekuwa akiendelea kuhoji suala hilo bungeni peke
yake bila kupata kuungwa mkono na kupewa msaada wa aina yoyote kutoka
kwa wenzake wa kambi ya upinzani bungeni.
Kamati ya Bunge ya
Hesabu za Serikali (PAC) ilielekeza kuwapo kwa ukaguzi maalumu kwenye
akaunti hiyo ya Tegeta escrow account iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania
(BoT) kwa kuwa ndani yake kulikuwapo fedha za umma. PAC haina sababu
yoyote ya kufuatilia fedha za watu binafsi. Mwaka 2009 iliyokuwa Kamati
ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) ilitoa maelekezo kwa BoT
kutothubutu kutoa fedha hizo. Agizo hilo la POAC lilitokana na sababu
kwamba fedha hizo zilikuwa ndani ya hesabu za Tanesco.
Akaunti ya
‘Tegeta escrow’ ilifunguliwa kutokana na kuwapo kutoelewana kuhusiana
na gharama halisi na halali za umeme unaozalishwa na IPTL na kuuzwa kwa
TANESCO. Mahakama ya Usuluhishi ya Kimataifa (ICSID) katika uamuzi wake
wa Februari, 2014 ilitoa hukumu kuonyesha kwamba Tanesco walitozwa
kiwango cha juu zaidi ya kilichopaswa kulipwa kwa IPTL. Kwa uamuzi huo
ni dhahiri kwamba fedha zilizokuwa zimehifadiwa kwenye akaunti hiyo
maalumu ya escrow zilipaswa kugawanywa kwa IPTL na Tanesco baada ya
hesabu kufanyiwa marekebisho upya kwa viwango halali.
Hesabu za
mwaka wa fedha ulioishia Disemba 2012 za Tanesco zinaonyesha wazi kwamba
fedha hizo ni mali ya shirika hilo la umma linalomilikiwa na serikali
kwa asilimia mia moja. Fedha za kampuni ni suala la kisheria kama
inavyobainishwa katika sheria ya kampuni ya mwaka 2002.
Kwa
maelezo hayo na hoja hizo, inakuaje serikali ianze kudai kwamba fedha
hizo si mali ya umma? Hivi inawezekanaje kwa fedha za mtu binafsi
zikaingizwa katika hesabu za shirika la umma linalomilikiwa na serikali
kwa asilimia 100? Ni lini fedha hizo zimekoma kuwa za umma? Je ni baada
ya baadhi ya watendaji wa serikali kula njama za kuzichukua fedha hizo
kwa kushirikiana na ‘mwekezaji’ aliyechafuka kwa ufisadi duniani?
Serikali inadanganya waziwazi kudai kwamba fedha hizo si mali ya umma.
Umma una haki ya kukumbushwa kwamba madai hayo yalitolewa pia katika
lile sakata la ufisadi maarufu wa EPA unaofanana kwa kila hali na huu wa
sasa wa ‘Tegeta Escrow’.
Hoja nyingine ni kwamba, Mbunge
Kafulila alisema kwamba Jaji Utamwa wa Mahakama Kuu ya Tanzania hakutoa
uamuzi wa kuchukuliwa fedha kutoka akaunti ya ‘Tegeta Escrow’. Nimepitia
kwa makini hukumu ya Jaji Utamwa na kubaini kwamba hakuna popote
alipotaja akaunti ya ‘Escrow’. Hata hivyo, nilipopitia muhstasari wa
kikao kati ya TANESCO, IPTL na Wizara ya Nishati na Madini, ndipo kwa
mara ya kwanza nikakuta wametafsiri uamuzi wa mahakama wakidai kwamba
fedha zote za ‘Tegeta Escrow’ zipewe kampuni ya PAP (inamilikiwa kwa
asilimia 50 na Harbinder Singh na 50% na Simba Trust iliyosajiliwa
Australia). Hiki ndicho kikao kilichofanya maamuzi ya kuiba na kugawana
wenyewe fedha hizo (Hukumu ya Jaji Utamwa na muhstasari wa kikao
vinaambatanishwa).
Wote waliohudhuria kikao hicho kilichojipa
mamlaka ya kutafsiri hukumu ya Mahakama Kuu, wanapaswa kuchunguzwa na
kufikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria zilizopo. Inawezekana vipi
uamuzi wa mahakama ukatafsiriwa na kikao cha Wizara? Muhstasari wa kikao
hicho ndio uliowasilishwa Benki Kuu (BoT) kuhalalisha madai kwamba
fedha hizo lazima zitolewa kutoka akaunti ya Escrow.
Fedha
zinazohusiana na akaunti ya Escrow ni Dola za Marekani milioni 250,
katia ya hizo Dola milioni 122 zilizokuwa BoT zimeshatolewa na kiasi
kilichosalia Dola milioni 128 zitalipwa na Tanesco kutokana na fedha
zake kwa madai ya kushindwa kulipa kwa wakati. Fedha zilizolipwa ni zile
ambazo zimetoka Wizara ya Nishati na Madini ambayo kisheria ndio
walipaswa kulipia gharama za uzalishaji umeme (capacity charge) fedha
zilizotoka kwa walipa kodi.
Ikumbukwe kwamba uhamishaji wa
asilimia 70 ya hisa za IPTL kwenda PAP umeambatana na nyaraka za
kughushi kutokana na kutokuwepo kabisa kwa uthibitisho wa cheti halisi
cha hisa (share certificate) kutoka kampuni ya Mechmar kwenda kampuni ya
Piperlink. Nyaraka za TRA zinaonyesha kwamba hisa hizo (70%) ziliuzwa
kwa Shilingi za Kitanzania milioni sita (6) tu. Na bado hakuna ushahidi
kuonyesha kwamba uhamishaji huo wa hisa ulipata baraka za mamlaka husika
kama inavyotakiwa na sheria za nchi.
Wakati huyo anayejiita
mmiliki mpya wa IPTL aliposaini mkataba wa kuchukua fedha kutoka akaunti
ya Escrow zilizokuwapo BoT, hakuwa mmiliki halali kisheria kwani kodi
ililipwa siku moja baada ya wao kupokea fedha kutoka BoT. Sheria inataka
kutolewa kwa cheti na Kamishna wa TRA kama uthibitisho kwamba kodi yote
imelipwa ipasavyo (Sheria ya Fedha ya 2012 kifungu cha 29).
Ni
nani wamiliki wengine wa kampuni ya PAP? Uchunguzi ni muhimu ukawalenga
vigogo na wanasiasa wakubwa wakiwamo watendaji waandamizi wa Wizara ya
Nishati na Madini.
Inapaswa tutafakari kuona kwamba Harbinder
Singh aliyechukua fedha za Escrow, anamiliki vitalu vya mafuta na gesi
kupitia kampuni iitwayo HydroTanz ambayo nayo imesajiliwa nchini
Australia, ikiwa na anwani sawa na ya kampuni ya Simba Trust. Kitalu
hicho cha mafuta kinaitwa ‘Mnazi Bay North’, jirani kabisa na ugunduzi
mkubwa wa hivi karibuni mkoani Mtwara.
Tunatarajia kwamba
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), atafichua ukweli wa sakata
hili na TAKUKURU itawafikisha mahakamani wahusika bila kujali nyadhifa
zao serikalini.
Kauli ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na
Madini, Eliakim Maswi, kwamba kuna watu waliokula rushwa na kwamba
nyaraka zinazotajwa ni karatasi za kuuzia vitumbua, ni kauli zenye
kuonyesha kutapatapa kwa watendaji serikalini. Hakuna hata mahali pamoja
ambapo nimemtaja mtu kuwa ni mwizi zaidi ya kuwasilisha hoja
zinazohitaji majibu mwafaka na si matusi, vitisho na tuhuma za kuzusha.
Nyaraka za TRA haziwezi kuwa za kufungua maandazi kama ambavyo hukumu ya
Jaji wa Mahakama Kuu haiwezi kuwa karatasi za kufungia maandazi na
badala yake ni nyaraka halali zinazohitaji maelezo kutoka kwa viongozi
na watendaji wa serikali badala ya kuropoka na kuporomosha matusi.
Hali kadhalika, Bunge lina kila sababu kupitia sheria yake ya Haki,
Maadili na Madaraka ya Bunge kulinda hadhi yake kutoka kwa watendaji
kama Maswi ambao wanatoa matamshi ya kuonyesha kwamba chombo hicho ni
chombo cha watu wasiofaa na kwamba watu wanaofaa wanazungumza nje ya
Bunge. Maswi na wengine kama wana ushahidi wa rushwa dhidi ya mbunge ama
yeyote hawapaswi kupayuka ovyo bali kwa nafasi zao wanaweza kuwasiliana
na vyombo vya dola kama TAKUKURU na polisi ili wachunguze na kuchukua
hatua kama ambavyo vinawachunguza wao.
Kauli ya Maswi kwamba
“wanaume” hawazungumzi ndani ya Bunge si tu udhalilishaji wa chombo
hicho bali pia inaashiria ugonjwa wa mfumo dume uliotawala miongoni mwa
viongozi wetu kwa maana kwamba wanaume ndio wenye hadhi, uwezo na
heshima na wanawake ni dhaifu na wasiostahili heshima. Tufumbue macho
tuone na tuondoe hisia binafsi zenye kubebwa na itikadi, chuki na
misimamo yetu ya kisiasa. Tuwe wazalendo ili tuweze kusimamia utaifa.
0 comments:
Chapisha Maoni