Jumapili, Juni 29, 2014

WENGINE 11 WAUAWA KATIKA SHAMBULIO NIGERIA

Nchini Nigeria watu wasiopungua 11 wameuawa baada ya mlipuko kujiri ndani ya hoteli moja katika mji wa Bauchi kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
Maafisa wa usalama katika eneo hilo wanasema mlipuko huo ambao pia uliwajeruhi karibu watu 30 ulijiri Ijumaa usiku wakati wateja walipokuwa wakitizama marudio ya mechi bora za Kombe la Dunia. Walioshuhudia wanasema washambuliaji waliokuwa wamevalia sare za kijeshi waliingia katika eneo hilo na kutega mabomu huku wakifyatua risasi kiholela. Jana Jumamosi Mkuu wa Polisi katika jimbo la Bauchi Lawal Shehu alisema kuwa mshukiwa mmoja ameshakamatwa kuhusiana na hujuma hiyo ya Ijumaa. Hakuna kundi lolote lililodai kuhusuka na hujuma hiyo lakini wakuu wa Nigeria kwa kawaida hulilaumu kundi la kitakfiri la Boko Haram kuwa ndio huhusika na vitendo kama hivyo vya kigaidi.
Katika miezi ya hivi karibuni mamia ya watu wameuawa nchini Nigeria kutokana na hujuma za kundi hilo la Boko Haram ambalo pia linawashikilia mateka mamia ya wasichana, wanawake na watoto.

0 comments:

Chapisha Maoni