Jumapili, Juni 29, 2014

WAMACHINGA DAR WAIBUA MAOFISA FEKI

Zoezi la kukamata Machinga linaloendelea Dar es Salaam, limesababisha kuibuka kwa maofisa na madalali feki wa jiji wanaochukua bidhaa za wafanyabiashara hao.
Zoezi hilo ambalo hulenga kusafisha jiji hilo lililokithiri kwa uchafu, limekuwa likikumbana na vikwazo mara kwa mara huku Machinga na baadhi ya wabunge wakihoji uhalali wake.
Uchunguzi uliofanywa na Fichuo umebaini kuwepo kwa kundi la watu linalojifanya kuwa ni maofisa kutoka ofisi za jiji, ambao linaendesha operesheni ya kuwatimua machinga wanaovunja sheria za biashara wakati wa usiku.
Wiki iliyopita gazeti hili liliripoti namna ambavyo zoezi la kukamata bidhaa za wafanyabiashara hao machinga, lilivyogeuka kuwa ‘neema’ kwa baadhi ya viongozi, ambao hugawana mali za thamani wanazozikamata.
Katika taarifa hiyo Chanzo cha habari hii kilishuhudia namna ambavyo uuzaji wa bidhaa zilizokamatwa zinavyopigwa kwa bei ndogo kwenye minada huku madalali wakichukua kila kitu wanachoona kinafaa.
Eliakunda Kira, anayefanya biashara katika Soko la Kariakoo alisema kuwa zoezi la kuwaondoa machinga limezaa maofisa feki ambao huonekana jioni wakiwatishia wafanyabiashara hao kuwa wasipotoa fedha watawapeleka ofisini ambako watalazimishwa kulipa Sh400, 000.
Kira alisema tayari kuna Machinga kadhaa wameshatumbukia mikononi mwa madalali na maofisa feki wanaosema wametumwa na jiji kukamata wafanyabiashara wanaovunja sheria.
Hata hivyo, akizungumza na Fichuo, Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe alisema kutokana na kuwepo kwa madalali wa jiji na Sumatra wanaokamata watu wanaofanya makosa mbalimbali mitaani na barabarani, wameibuka madalali feki wanaotakiwa kudhibitiwa.
Sumatra wanakamata magari yanayobeba abiria wakati hayana kibali cha kufanya hivyo, lakini madalali wa jiji wao wanahusika na mambo mengine ikiwemo kukamata magari yaliyoegeshwa vibaya
alisema Kabwe na kuongeza kuwa: “Mtu anayekamatwa na madalali lazima ahakikishe anaonyeshwa kitambulisho.”
Mfanyakazi mmoja wa kampuni ya udalali ambaye hakutaka kutaja jina lake, kwa kuhofia kupoteza kazi, alisema kuwa baadhi ya kampuni za udalali jijini Dar es Salaam zinamilikiwa na vigogo waliopo serikalini, jambo linalofanya kazi ya kuziwajibisha kuwa ngumu.

0 comments:

Chapisha Maoni