Kikao cha kwanza cha Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEA),
kimehitimishwa mjini Nairobi, Kenya kwa wito wa kutaka hatua
zichukuliwe ili kuboresha usafi wa hewa na kuzuia vifo milioni 7 vya
mapema ambavyo hutokana na hewa chafu. Kikao hicho cha siku tano
kilihitimishwa Ijumaa kwa kupitisha maazimio 16 yanayohimiza hatua za
kimataifa katika kukabiliana na masuala kadhaa yanayohusu mazingira,
yakiwemo yanayohusiana na biashara haramu ya viumbe wa porini, usafi wa
hewa, taka za plastiki katika bahari, kemikali na taka kwa ujumla.
Akizungumza wakati wa kufunga kikao hicho, Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa, Ban Ki-Moon, alisema kuwa hewa tunayopumua, maji tunayokunywa
na udongo tunamozalishia chakula, ni sehemu ya bayo anuai ambayo
inaendelea kukabiliwa na shinikizo kubwa. Baraza hilo lilitambulisha
uchafuzi wa hewa kama tatizo linalopaswa kupewa kipaumbele na jamii ya
kimataifa, ili kuepusha vifo milioni 7 kila mwaka, kwa mujibu wa takwimu
za Shirika la Afya Duniani, WHO. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
iliwakilishwa katika mkutano huo na makamu wake wa rais ambaye pia ni
Mkuu wa Shirika la Mazingira Iran Dkt. Maasoumeh Ebtekar. Akiwa nchini
Kenya Bi. Ebtekar pia alikutana na kufanya mazungumzo naProf. Judi
Wakhungu Waziri wa Mazingira, Maji na Mali Asili wa Kenya ambapo
walijadili masuala ya kimataifa na ushirikiano wa Tehran na Nairobi
katika masuala ya mazingira, ustawi endelevu na utalii wa kimazingira
yaani Eco-tourism.
0 comments:
Chapisha Maoni