Ofisa ustawi wa jamii Mkoa wa Morogoro, Oswin Ngungatuti alisema mwili wa mtoto huyo utasafirishwa leo kwenda Morogoro.
Ngungamtitu alisema mazishi ya Nasra yatatanguliwa
na ibada itakayoambatana na utoaji wa heshima za mwisho katika Uwanja
wa Jamhuri, hatua ambayo alisema inatokana na baba mzazi wa mtoto huyo,
Rashid Mvungi kuwa mmoja wa watuhumiwa wa mateso yake.
Hata hivyo, Mvungi licha ya kushiriki vikao vilivyopanga mazishi
ya Nasra, jana alisema angefurahi kama angepewa mwili wa mtoto wake ili
auzike mwenyewe badala ya kuzikwa na Serikali.
Tayari mimi na familia yangu akiwamo mke wangu tulishakubaliana kumlea na nilipanga baada ya kupona niwaombe ustawi wa jamii ili nimlee mwenyewe, lakini leo nilipopata taarifa hizi kwa kweli nimechanganyikiwa na sijui cha kufanya.
Katika kikao cha mazishi, Mkurugenzi wa Kampuni ya
Mabasi ya Al Saed, Omary Al Saed alisema kampuni yake itatoa gharama
zote za mazishi kuanzia kusafirisha mwili wa marehemu kwenda Morogoro na
gharama nyingine.
Wadau wengine ambao walitoa michango yao ni
Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Morogoro (MRFA), Pascal Kianga na
Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro.
Mateso ya Nasra
Nasra alifichwa katika boksi na mama yake mkubwa, Mariam Said mkazi wa Uwanja wa Ndege, Morogoro tangu akiwa na miezi tisa.
Alianza kumlea mtoto huyo baada ya mdogo wake
ambaye ni mama yake Nasra kufariki dunia. Majirani wa Mariam ndiyo
waliotoa taarifa za kuwepo kwa mtoto huyo baada ya kumsikia akilia na
kukohoa nyakati za usiku.
Mwanamke huyo, Mvungi na mume wa Mariam, Mtonga
Omar wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Morogoro kujibu
mashtaka ya kula njama na kufanya ukatili dhidi ya mtoto huyo.
Jana Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro,
John Laswai alisema kutokana na kifo cha Nasra, mashtaka dhidi ya
watuhumiwa yanaweza kubadilika, lakini mabadiliko hayo yatategemea
ripoti ya daktari kuhusu sababu za kifo hicho.
Laswai alisema taratibu za kipolisi zinafanywa
kuwezesha kupatikana kwa taarifa hiyo, ambayo itapelekwa kwa wanasheria
ambao baada ya kuipitia wanaweza kuwa na mapendekezo ya kubadili
mashtaka dhidi ya watuhumiwa hao.



0 comments:
Chapisha Maoni