Jumatatu, Juni 30, 2014

MFUNGO WA RAMADHAN WAPANDISHA BEI ZA VYAKULA!

KUTOKANA na kuanza kwa Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, baadhi ya wafanyabiashara katika mikoa mbalimbali nchini, wamepandisha bei za vyakula, hali iliyoanza kuleta usumbufu kwa wananchi. Chanzo kilitembelea masoko kadhaa katika mikoa ya Dar es Salaam, Zanzibar na Shinyanga jana na kubaini kuwa bei za vyakula, zimepanda maradufu mara tu baada ya Mfungo kuanza juzi.
Masoko yaliyotembelewa jijini Dar es Salaam ni Buguruni, Tandale, Kariakoo, Urafiki na Makumbusho. Viongozi mbalimbali akiwemo Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salam, Alhad Mussa Salum walikemea hatua hiyo ya kupandisha bei vyakua. Ilibainika kuwa vyakula ambavyo bei yake imepanda ndani ya siku mbili zilizopita ni zile zinazotumiwa kwa futari, ikiwemo mihogo, viazi , ndizi, magimbi, mchele na vinginevyo ambapo tofauti na siku za nyuma kwa sasa uuzwaji wake umekuwa wa tofauti.
Ukichukulia mfano wa viazi vitamu na mihogo, fungu ambalo kabla ya kuanza kwa Mwezi Mtukufu, lilikuwa likiuzwa kwa Sh 1000, hivi sasa limepandishwa na bei hadi kufikia Sh 2000.
Pia, mkungu wa ndizi uliokuwa ukiuzwa kwa Sh 6,000 hadi 7,000 kwa sasa umepanda bei hadi kufikia Sh 10,000, jambo linaloashiria limechangiwa na mahitaji makubwa ya wanunuzi.
Wakizungumza na chanzo kuhusu hali hiyo, baadhi ya wafanyabiashara katika soko maarufu la vyakula la Urafiki, walikiri kupanda kwa bidhaa hizo.
Pia, walisema hatua hiyo imesababishwa na uhaba wa vyakula hivyo kwa sasa.

0 comments:

Chapisha Maoni