Jumapili, Juni 29, 2014

KUFIKIA 2027 TANZANIA HAKUTAKUWA NA WATU VIJIJINI, RIPOTI YA BENKI YA DUNIA IKO HAPA

Katika kusoma ripoti ya Benki ya Dunia juu ya hali ya Uchumi wa nchi yetu Tanzania, nimevutiwa na nimeona si vibaya niliwasilishe hapa ili tubadilishane mawazo ya kile ambacho tayari tunakielewa, kile kilichopo katika ripoti kama tunakubali au kukataliana nacho na msingi zaidi ni tokana na hali ya Uchumi wetu, mitazamo yetu binafsi ipo vipi?
Benki ya Dunia (World Bank) hivi karibuni imetoa Ripoti ambayo imeonyesha taswira ya kuongezeka kwa idadi ya Watanzania katika miji mikubwa kuliko vijijini. Ripoti hii inaonyesha pia hali ya uchumi ilivyokuwa miaka michache ya nyuma, uchumi ulivyo sasa na utakavyokuwa ifikapo 2030. Kumekuwa na kuongezeka kwa kasi ya watu wanaohamia miji mikubwa hadi inaaminika kuwa kuna hatihati ya vijiji kuwa ‘Depopulated’ na kubaki watu wachache hadi kufanya vijiji hivyo kushindwa kujiendesha.
  Katika ripoti hiyo, kuna baadhi ya haya ambayo yanazua mjadala:
=> Ifikapo mwaka 2027, Watanzania wengi zaidi inadaiwa watakuwa wanaishi katika maeneo ya mijini kuliko vijijini, na Dar es Salaam litakuwa jiji kuu likiwa na watu zaidi ya milioni 10.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa hili si jambo baya; Maadam changamoto zinazotokana na kukua kwa idadi hiyo zikishughulikiwa kupitia utekelezaji wa sera nadhifu zinazowezesha ukuaji chanya katika maeneo ya mijini. Kuongezeka kwa msongamano wa watu katika maeneo ya mijini pia huhitaji utoaji wa miundombinu ya kutosha ya kijamii na huduma kama vile barabara, maji, umeme n.k. Kwa bahati mbaya, katika maeneo yote haya, Tanzania iko katika hatari ya kubaki nyuma.
=> Kutokana na kugunduliwa hivi karibuni kwa akiba kubwa ya gesi asilia, Tanzania imeendelea kuwavutia wawekezaji wa kimataifa. Tanzania inaweza kubaki katika njia ya ukuaji uchumi chanya hadi siku za baadaye, ilimradi Serikali iimarishe nakisi yake ya fedha. Ukuaji uchumi uliokadiriwa kubakia takribani asilimia 7, utapaswa kuendelea kusukumwa na sekta zile zile ambazo zinapanuka haraka kama ilivyokuwa kwa miaka iliyopita. Kiwango cha mfumuko wa bei kinatarajiwa kubakia takribani asilimia 5 kwa mwaka, ilmradi uchumi hauathiriki na misukosuko ya bei za chakula na nishati. Ripoti hii imeiweka Tanzania katika nafasi ya juu (iliongoza) Afrika Mashariki kwa ukuaji wa uchumi kwa mwaka 2013.

=> Sehemu kubwa ya biashara za mijini ambazo sio za kilimo ni ndogo, changa, tete, sio rasmi na si za kitaalamu, na huendeshwa na wenye mali ambao wana ujuzi mdogo. Wamiliki wa biashara hizi wameelezewa kuwa ni ‘wajasiriamali wasio na ari’ kwani mara nyingi huanzisha biashara kwa sababu moja tu, kwamba hawana njia nyingine ya kujikimu! Aidha, ni asilimia 40 tu ya biashara mlga zinazoanzishwa ndizo huweza kuhimili mikikimikiki ya changamoto za soko; asilimia 60 ya biashara hizo hufa muda mfupi baada ya kufunguliwa.

=> Msongamano wa Magari jijini Dar una athari kubwa kwa uchumi wa nchi. Wakazi wengi wa Dar hutumia takribani asilimia 34 ya kipato chao cha mwezi kwa ajili ya usafiri tu!

0 comments:

Chapisha Maoni