Watu saba wakiwamo mameneja wawili wa Benki ya Barclays
wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na
mashtaka ya wizi wa zaidi ya Sh479 milioni mali ya benki hiyo.
Akiwasomea hati ya mashtaka yanayowakabili
washtakiwa hao, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumain Kweka
akishirikiana na wakili mwenzie wa serikali Mwanaamina Kombakono
waliwataja washtakiwa hao kuwa ni Meneja wa benki hiyo Tawi la
Kinondoni, Alune Kasililika (28).
Washtakiwa wengine ni Meneja Neema Batchu,
wafanyabiashara Kakamie Julius (32), Iddy Khamis (32), Sezary Massawe
(31), Boniphace Muumba (29) na Ruth Macha (30).
Kweka alidai kuwa siku ambayo haifahamiki
washtakiwa hao kwa pamoja wakiwa jijini Dar es Salaam walipanga njama
ya kutenda kosa hilo la wizi.
Alidai kuwa Aprili 15, katika Benki ya Barclays
Tawi la Kinondoni, washtakiwa hao waliiba Sh390,220,000, dola za
Marekani 55,000 na Euro 2,150.
Wakili huyo wa Serikali aliendelea kudai kuwa
kabla ya washtakiwa hao kufanikisha wizi huo, waliwaua wafanyakazi wa
benki hiyo ya Barclays Anifa Ahmad na Anna Tegete ili waweze kuzichukua
fedha hizo kwa urahisi.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo yanayowakabili,
washtakiwa wote waliyakana na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi
wa kesi hiyo bado haujakamilika.
Hakimu Mkazi, Nyigulile Mwaseba aliiahirisha kesi
hiyo hadi Mei 15,na kuamuru washtakiwa hao kupelekwa rumande kwa kuwa
mashtaka yanayowakabili ni moja kati ya mashtaka yasiyo na dhamana
kisheria.
0 comments:
Chapisha Maoni