Siku kama ya leo miaka 8
iliyopita, inayosadifiana na tarehe 20 Farvardin 1385 Jamhuri ya
Kiislamu ya Iran ilifanikiwa kupata teknolojia ya kurutubisha madini ya
urani kwa ajili ya matumizi ya kiraia. Wasomi na wataalamu wa Iran
walifanikiwa kukamilisha mfumo wa kuzalisha nishati ya nyuklia licha ya
mbinyo na vikwazo vya nchi za kibeberu. Kwa utaratibu huo Iran iliingia
katika kundi la nchi zenye teknolojia ya nyuklia duniani. Mwaka mmoja
baadaye Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilianza kuzalisha nishati hiyo
viwandani. Mafanikio hayo makubwa ya Iran yalipatikana chini ya
usimamizi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA). Hata
hivyo baadhi ya nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani zinapinga
vikali miradi ya nishati ya nyuklia ya Iran kutokana na sera zao za
kindumakuwili na za kibaguzi.
Tarehe 9 Aprili miaka 11
iliyopita, mji mkuu wa Iraq Baghdad ulitekwa na majeshi ya Marekani na
waitifaki wake na utawala wa Saddam Hussein ukasambaratika. Marekani
ilianza kuishambulia Iraq tarehe 20 Machi mwaka 2003 na ilitazamiwa
kwamba jeshi hilo vamizi lingekabiliwa na upinzani mkali wa majeshi ya
Iraq mjini Baghdad. Lakini la kushangaza ni kuwa askari wa Marekani
waliingia mjini humo bila ya kukabiliwa na upinzani mkali. Tangu wakati
huo Washington imekuwa ikipora utajiri wa Iraq hususan maliasili ya
mafuta ya nchi hiyo na kufanya jitihada zaidi za kudhibiti nchi nyingine
za Mashariki ya Kati.
Na siku kama ya leo miaka 66
iliyopita utawala ghasibu wa Israel ulifanya mauaji ya kinyama katika
kijiji cha Deir Yassin huko magharibi mwa Baitul Muqaddas. Mauaji hayo
yalifanyika wakati wa vita vya kwanza vya Waarabu na Israel na
yalitekelezwa na Wazayuni wa kundi la Irgun lililokuwa likiongozwa na
waziri mkuu wa zamani wa Israel Menachem Begin. Eneo la Dier Yassin
lilikuwa na umuhimu mkubwa kwa Wazayuni kutokana na kuwa katika njia ya
Baitul Muqaddas na karibu na pwani. Baada ya kukivamia kijiji cha Deir
Yassin, Wazayuni hao waliwaua kinyama wakazi 270 ambao hawakuwa na hatia
yoyote wa kijiji hicho. Mauaji hayo yaliwalazimisha Wapalestina wengi
wa eneo hilo kukimbia makazi yao kwa kuhofia kukaririwa mauaji kama hayo
ya kinyama.



0 comments:
Chapisha Maoni