Polisi nchini Malaysia wamevamia nyumba aliyokuwa akiishi rubani
wa ndege iliyopotea na kuendesha msako mkali, ikiwamo kukusanya nyaraka
muhimu ambazo zinazamiwa kuwa zitasaidia kufichua ukweli kuhusu tukio
la kupotea kwa ndege hiyo.
Ripoti zilisema kuwa upekuzi huo, ambao pia
umefanyika katika nyumba aliyokuwa akiishi rubani msaidizi, umefanyika
baada ya kuibuka kwa taarifa zinazodai kuwa rubani huyo, Zaharie Ahmad
Shah alikuwa na mrengo wa siasa kali.
Shah alikuwa ni shabiki na mfuasi wa wazi wa
mwanasiasa wa upinzani, Anwar Ibrahim ambaye sasa yupo gerezani baada ya
kukutwa na hatia ya kujihusisha na vitendo vya fedheha.
Inaaminika kuwa rubani huyo alikuwapo mahakamani
wakati mwanasiasa huyo alipopandishwa kizimbani mwezi Machi mwaka huu na
pengine hakufurahishwa na hukumu hiyo.
Kwa sasa polisi wanashikilia nyaraka kadhaa,
ikiwamo kompyuta ambayo inadhaniwa kuwa na taarifa muhimu
zilizohifadhiwa na rubani huyo.
Polisi hao wameenda mbali zaidi kwa kuanzisha
uchunguzi wa kimazingira ambao utasaidia kupata historia binafsi kuhusu
maisha ya rubani huyo aliyetajwa kuwa na uzoefu mkubwa wa urushaji wa
ndege.
Wataalamu wa saikolojia na wale wanaohusika na
usalama wa anga wameitwa kuongeza nguvu ili kusaidia kuchambua taarifa
zinazoendelea kukusanywa kuhusu mwenendo wa rubani Shah ambaye nyumba
yake bado inaendelea kulindwa.
Kitendo cha polisi kuifanyia upekuzi nyumba ya
rubani huyo pamoja na kukusanya taarifa zake binafsi kimeelezwa kwamba
ni jitihada za Serikali kutaka kujiridhisha hasa kutokana na mazingira
yanayohusisha upotevu wa ndege hiyo.
Wachunguzi hao wanataka kujua kama kumekuwa na
tukio lolote la matatizo ya kiakili na kumewahi kujitokeza kwa
changamoto za kifamilia kwa marubani hao au kwa yeyote aliyekuwamo
kwenye ndege hiyo iliyokuwa ikisafiri kutoka Kuala Lumpur na kuelekea
Beijing.
Pamoja na kwamba marubani wa ndege hiyo ya
Malaysia walikuwa na rekodi nzuri, kuna wasiwasi pengine walikutwa na
tukio lililosababisha kujiingiza kwenye hali ambayo ingepoteza umakini
wa kuongoza ndege.
Uchunguzi pia unawalenga abiria waliokuwemo kwenye
ndege hiyo iliyokuwa na umri wa miaka 11 na kwamba hatua hiyo inaweza
kusaidia upatikanaji ukweli halisi juu ya tukio hilo.
0 comments:
Chapisha Maoni