Mji wa Hedaru uliopo wilayani Same mkoani Kilimanjaro, jana
ulizizima kwa vilio na simanzi baada ya waombolezaji 12 wote ndugu,
kufariki dunia kwa ajali ya barabarani.
Waombolezaji hao wanawake, walipewa lifti ya gari
na Diwani wa Kata ya Hedaru, Gerard Mgwena (CCM), kwa ajili ya
kuwapeleka msibani eneo la Majengo ambako mtu mmoja alifariki kwa
kusombwa na maji.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro (RPC),
Robert Boaz alithibitisha ajali hiyo akisema ilitokea juzi saa 2:00
usiku na kwamba ilikuwa mbaya zaidi tangu kuanza kwa mwaka 2014.
“Ni ajali iliyohusisha magari matatu kwa wakati
mmoja…; watu 11 walifariki pale pale na mwingine alifariki dunia leo
(jana), asubuhi Hospitali ya Rufaa ya KCMC,”alisema Boaz.
Hata hivyo, alisema hakuwa na nafasi nzuri ya
kufafanua kwa undani ajali hiyo kwa vile alikuwa nje ya Mkoa wa
Kilimanjaro na kuelekeza atafutwe Kamanda wa Kikosi cha Usalama
Barabarani Mkoa (RTO), Joseph Mwakabonga.
Akizungumza kwa niaba ya RPC, Mwakabonga alisema,
lori aina ya Mitsubish Fusso lililokuwa likitokea Moshi kwenda Dar
liligonga kwa nyuma gari aina ya Toyota Hilux Pick-Up.
Alisema kuwa baada ya kuligonga gari hilo
lililowabeba waombolezaji hao, nalo lilisukumwa na kwenda kuligonga lori
aina ya Scania lililokuwa na tela lake.
Lori hilo aina ya Scania lilikuwa likitokea Dar es
Salaam kwenda Moshi likiendeshwa na dereva wake, Gabriel David.
Madareva wawili wa Toyota Pick-Up na Toyota Fusso wote hawajulikani
waliko.
Taarifa zilizopatikana baadaye, zilisema dereva wa
Fusso alikuwa amelazwa katika Hospitali ya KCMC, wakati Kigogo wa CCM
aliyekuwa amewabeba waombolezaji akilazwa hospitali moja jijini Arusha.
Mwakabonga aliwataja waliofariki kuwa ni Stella
John(45), Salma Kizoka (33), Marry Senzige (49), Neema Daniel (52),
Rehema George (29) na Sophia Mbike (51).
Wengine ni Ritha Kalani (55), Mama Kalani Stephano
(55), Kolina Mmatha(55), Bahati Daud(25) na Farida Kiondo mwenye umri
wa miaka 25.
Majeruhi mmoja, Maria John (33) ambaye ni miongoni
mwa watu 10 waliojeruhiwa, alifariki dunia jana asubuhi katika
Hospitali ya Rufaa ya KCMC alikolazwa kwa ajili ya kuokoa maisha yake.
0 comments:
Chapisha Maoni