Jumanne, Machi 18, 2014

MSANII WA BONGO MOVIE YU HOI, ANAHITAJI MAOMBI YA WATANZANIA

Hali ya kiafya ya msanii wa Komedi Bongo, Ismail Issa Makombe ‘Mapembe’ inazidi kuwa mbaya kutokana na kuugua maradhi ya ini kwa muda mrefu huku ikidaiwa kuwa wasanii wenzake wamemtelekeza.
Mapembe ambaye anapiga mzigo katika Kampuni ya Al-Riyam inayozalisha kipindi cha vichekesho cha Vituko Show kinachorushwa kwenye Runinga ya Channel Ten, amelia  kuwa anateseka na ugonjwa huo tangu mwaka jana.
Msanii huyo alifunguka kwamba alipimwa katika Hospitali ya Burhan, Dar na kuambiwa kuwa mwili wake umejaa sumu kwa asilimia 93 na ini limefeli huku akiwa ametokwa na vidonda usoni na tumbo lake kuvimba.

“Nimeamua kurudi nyumbani kwetu Mtwara ili angalau niombe msaada kwa ndugu na jamaa zangu niweze kuishi na kujaribu kupata matibabu zaidi.

“Hali yangu ni mbaya sana kwani mwanzo nilikuwa nikisaidiwa na bosi wangu ambaye naye kwa sasa anaonekana kuelemewa na majukumu yake, hivyo nawaomba sana wadau  waweze kunisaidia kwa sababu ninaumia sana.
“Imefikia hatua leo ninatambua kuwa wasanii wa filamu ni wanafiki, maana tangu mwaka jana hadi leo ninaumwa lakini hakuna hata mmoja aliyeweza kunisaidia zaidi ya Kitale ambaye alikuja kuniona,” alisema.

Mapembe kabla hajaugua alikuwa akiigiza kwenye Kundi la Vituko Show  kwa kuvaa uhusika wa aina mbalimbali lakini mara nyingi alikuwa akifiti sana alipokuwa akiigiza kama askari wa usalama barabarani ‘trafiki’.

0 comments:

Chapisha Maoni