MWANAMUZIKI mkongwe nchini, Nguza Viking ‘Babu Seya’
anayetumikia kifungo cha maisha jela na mwanaye Johnson Nguza ‘Papii
Kocha’ kwa kuwanajisi watoto tisa, wana furaha upya baada ya mwanga wa
kuweza kurudi uraiani kuchomoza tena, wakili wao, Mabere Nyaucho Marando
amezungumza na Uwazi.
KASORO HUKUMU YA MWANZO Akizungumza juzi jijini Dar
es Salaam, Marando alisema kwamba katika kesi ya Babu Seya na mwanaye
iliyosikilizwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar aligundua
kuna vielelezo muhimu ambavyo havikuambatanishwa hivyo kuwa vigumu kwake
kuviingiza na kuvitetea katika ngazi ya mahakama ya rufaa
iliyoshindilia adhabu dhidi ya wawili hao.
Marando alisema mwanga mwingine wa kupitiwa upya wa mashitaka yao
umekuja baada ya kuwepo kwa kesi mpya inayofanana na ya akina Babu Seya
kwa asilimia mia moja. Alisema kesi hiyo ipo kwenye hatua ya mwisho
ambapo ushindi wake utamfanya apate nguvu ya kurudi mahakamani kuwatetea
wafungwa hao waliohukumiwa mwaka 2004.
DIRA KWENYE KESI HIYO “Kuna kesi mahakama kuu kanda
moja nchini inayotetewa na wakili maarufu (jina tunalo). Hii kesi
inafanana sana na ya akina Babu Seya. Uzuri wake ina dalili zote za
washtakiwa kuibuka na ushindi wa kishindo. MAHOJIANO Mazungumzo kati ya
Marando na Uwazi yalikuwa hivi:
Uwazi: Lakini mheshimiwa kesi ya Babu Seya si ilifika katika rufaa
mara tatu na wakashindwa na ulisema hakuna namna tena, sasa itakuwaje
kurejeshwa tena huko? Marando: Ni kweli, lakini ni jambo linalowezekana.
Nimesema kama hiyo kesi ninayoitaja watashinda na wanaweza kushinda,
basi mimi nitaenda kwa Nguza na kumwambia wazo langu, akikubali
nitaiandikia barua mahakama ya rufaa kuomba kupitiwa tena kwa yale
mashitaka, nitajenga hoja.
Uwazi: Hiyo kesi unayoingoja hukumu yake inahusu nini? Marando:
Inahusu kubaka na kulawiti, ni kama hii ya Babu Seya na wanawe. Hakuna
tofauti. Sasa washitakiwa wale wakishinda ndipo hoja inapokuja, kwa nini
vipengele vilevile viwatie hatiani akina Babu Seya wengine viwaweke
huru, ndivyo inavyokuwa katika kesi. Uwazi: Ukiwaandikia mahakama ya
rufaa wakakubali, majaji walewale watasikiliza ombi lako?
Marando: Hilo ni la mahakama lakini idadi inaweza kuongezwa na
kufikia majaji sita au saba.Uwazi: Una hakika utashinda na kukubaliwa?
Marando: Kama nilivyokueleza, ikipita ile kesi halafu mahakama ya rufaa
wakakubali kupitia tena jalada, nina uhakika wa kushinda.
ANALIPWA NA NANI? Wakili huyo maarufu alisema yeye aliwatetea
wanamuziki hao bure kwenye kesi yao ikiwa katika ngazi ya mahakama ya
rufaa baada ya kusoma jalada lenye kurasa 1,362 ambapo aligundua kuwa
kuna nyaraka kadhaa ambazo hazikuambatanishwa katika Mahakama ya Kisutu
ambazo zingeweza kuwaokoa na kifungo wateja wake.
“Unajua kesi inapokuwa mahakama ya rufaa, majaji wanachofanya ni
kupitia jalada si kusikiliza, hivyo haiwezekani kuambatanisha vielelezo
vipya,” alisema Marando ambaye anajipambanua kuwa awali alishinda nusu
kwa kuwatoa nje watoto wa Babu Seya, Mbangu na Francis Nguza ambao nao
walihukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kosa moja na wafungwa hao.
HUKO NYUMA Juni 25, 2004 Hakimu Mkuu Mkazi wa
Mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam, Addy Lyamuya aliwatia hatiani kwa
ubakaji na ulawiti Babu Seya na wanawe Papii Kocha, Mbangu na Francis.
Januari 27, 2005, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Thomas
Mihayo alitupilia mbali rufaa yao iliyokuwa ikipinga hukumu hiyo.
Wakili Marando akapeleka suala hilo Mahakama ya Rufaa Tanzania ambako
Mbangu na Francis waliachiwa huru na yeye kutangaza kwamba ameshinda
nusu. Babu Seya na wanawe walidaiwa kutenda makosa 10 ya kubaka na
kulawiti watoto hao kati ya Aprili na Oktoba 2003 katika maeneo ya Sinza
ya Kwaremmy, Dar es Salaam.
0 comments:
Chapisha Maoni