Alhamisi, Machi 20, 2014

BREAKING NEWS: WANAFUNZI WAVAMIA NA KUTEKA BUNGE

Mamia ya wanafunzi nchini Taiwan wamevamia na kuliteka bunge la nchi hiyo tangu Jumanne usiku kupinga kile wanachosema ni mkataba wa kibiashara kati ya nchi hiyo na China.
Ikiwa mkataba huo uliopitishwa mwaka jana utaidhinishwa , utaruhusu nchi hizo mbili kushirikiana na kuekeza katika sekta za huduma.

Mkataba huo unakuja wakati uhusiano kati ya nchi hizo mbili zilizokuwa zinahasimiana tangu mwishoni mwa vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1949 ni mzuri sana .
Lakini baadhi ya raia nchini Taiwan wana wasiwasi kuhusu nchi yao kutegemea sana China kiuchumi.
Mamia ya wanafunzi walizuia mlango wa bunge kwa viti na kujifungia ndani ya bunge hilo, wakilaani vikali mkataba huo.
Walivunja kizuizi kilichowekwa na polisi usiku na sasa wameteka chumba cha vikao vya bunge hilo.
Mamia ya wanafunzi wengine walikusanyika nje ya bunge kuwapa motisha vijana walio ndani ya bunge.
Wanafunzi hao wanasema kuwa serikali ilifikia mkataba huo na China bila ya kushauriana na wananchi. Wanasema wanahofia kuwa mkataba wenyewe utaathiri pakubwa wafanyabiashara wadogo wadogo pamoja na maisha ya wananchi wa kipato cha chini.
Pia wanahofia kuwa kisiwa hicho huenda kikashinikizwa kujiunga tena na China jambo ambalo wanapinga vikali.

0 comments:

Chapisha Maoni