Jumatatu, Machi 10, 2014

BAADA YA MGOGORO NA TANZANIA, SASA RWANDA YAINGIA KATIKA MGOGORO MPYA NA AFRIKA KUSINI

Serikali ya Afrika Kusini inafikiria uwezekano wa kuvunja kabisa uhusiano wake wa kidiplomasia na Rwanda, baada ya serikali ya Kigali kukumbwa na tuhuma za kufanya njama za kutaka kumuua mmoja wa makamanda wa zamani wa jeshi la Rwanda nchini Afrika Kusini.
Duru za kidiplomasia kutoka Afrika Kusini zinaeleza kuwa, serikali ya Pretoria inaangalia upya uhusiano wake wa kidiplomasia na Kigali na kuna uwezekano wa kurudishwa nyumbani balozi wa Afrika Kusini aliyeko Kigali , na ubalozi wa Rwanda kufungwa mjini Pretoria. Hivi karibuni, Afrika Kusini iliwatimua wanadiplomasia watatu wa Rwanda wanaoshukiwa kupanga njama za kumuuwa Jenerali Kayumba Nyamwasa, kamanda wa zamani wa Rwanda aliyeko uhamishoni nchini Afrika Kusini. Rwanda nayo katika radiamali yake iliamua kuwatimua wanadiplomasia sita wa Afrika Kusini walioko Kigali. Imeelezwa kuwa, uhusiano wa pande mbili ulianza kuingia dosari tarehe 3 Machi mwaka huu, baada ya watu wenye silaha kuvamia nyumba ya Jenerali Nyamwasa mjini Johannesburg na kupora mali kadhaa zikiwemo nyaraka na kompyuta mpakato. Wakati wa uvamizi huo, Jenerali Nyamwasa hakuwemo nyumbani. Inafaa kuashiria hapa kuwa, mwezi Disemba 2013 Kanali Patrick Karegeya mkuu wa zamani wa idara ya upelelezi ya Rwanda, aliuawa katika mazingira ya kutatanisha nchini Afrika Kusini.

0 comments:

Chapisha Maoni