SERIKALI ya Mkoa wa Iringa imeagiza kukamatwa kwa wanawake wanaouza miili (ukahaba) na wanaume mashoga
Agizo
hilo limetolewa hivi karibuni katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya
Mkoa wa Iringa kilichofanyika katika Ukumbi wa Siasa ni Kilimo chini ya
mkuu wa mkoa huo, Christine Ishengoma.
Hayo yamekuja baada ya Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya
Iringa, Amani Mwamwindi kuwaeleza wajumbe kuwa mbali ya kusikia kutoka
majiji kama Dar na mengine nchini kwamba biashara za ukahaba na ushoga
ziko juu, uchunguzi unaonesha mji wa Iringa ni miongoni mwa miji ambayo
biashara hiyo inaendelea kukua kwa kasi.
“Ndugu wajumbe, Manispaa ya Iringa ina watu wanaofanya biashara ya
ushoga na ukahaba. Mimi meya nina ushahidi wa kutosha. Idara
inayohusika na vita dhidi ya Ukimwi katika halmashauri ya manispaa
inaujua mtandao mzima wa biashara hiyo haramu,” alisema meya huyo.
Kufuatia ushahidi huo kutoka kwa meya, mkuu huyo wa mkoa alilazimika
kusimama na kuwataka wahusika kuwakamata watu hao wote ili ikibidi
wasaidiwe kupewa miradi rafiki badala ya kuendelea na biashara hiyo
haramu.
“Tusiwaache wapotee, tuwashike na kuwakusanya. Hawa ni Watanzania
wenzetu, yawezekana kuwapa elimu ili kuachana na shughuli hizo. Pia
kuwapa miradi ya kufanya kwa ajili ya kuwaingizia kipato na si kwa
shughuli hiyo,” alisema mkuu huyo wa mkoa.
0 comments:
Chapisha Maoni