Kesi ya Mtanzania Stephen Ongolo anayeshikiliwa na polisi Afrika
Kusini akituhumiwa kutishia kutoa siri za mke wa pili wa Rais wa nchi
hiyo, Jacob Zuma, Nompumelelo Ntuli Zuma (MaNtuli), imeibua mabishano ya
kisheria ya kuhusu mahali anapotakiwa kushtakiwa.
Gazeti la The Star la Afrika Kusini liliripoti
kuwa baada ya Ongolo kupandishwa kizimbani kwenye Mahakama ya Camperdown
jijini Durban, Jumatatu wiki hii, ilibainika kuwa Mwendesha Mashtaka wa
Serikali, Ndoda January hakueleza ni wilaya gani ya kimahakama ambayo
Ongolo alitenda kosa hilo. January alisema kuwa walishindwa kujua eneo
alilofanya makosa Ongolo, kwani alikuwa akitumia ujumbe mfupi wa simu
alioutuma kwa vyombo vya habari vya nchi hiyo.
“Tunashindwa kuelewa eneo gani ambalo mshtakiwa
amefanya kosa kwa sababu mlalamikaji anaweza kuwa sehemu yeyote kati ya
Camperdown na Nkandla ambako alipeleka ujumbe huo,” alisema January.
Kukamatwa kwa Ongolo
Ongolo alikamatwa na polisi jijini Durban mwezi
uliopita kwa madai ya kumtishia mke wa pili wa Rais Zuma kuwa angetoa
siri zake. Siri hizo zinahusiana na kifo cha mlinzi wa Rais Zuma, Phinda
Thomo, ambaye alidaiwa kujiua bafuni kwake mwaka 2009.
Ongolo alikaririwa na Gazeti la Sunday Independent
la Afrika Kusini akieleza kuwa Thomo hakujiua bali kifo chake
kilipangwa baada ya siri kati yake na MaNtuli kubainika.
Gazeti la The Star la nchini humo, jana liliripoti
kuwa hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Thys Talijaard wa Camperdown
alisema ili Ongolo apate dhamana hapo Camperdown, alitakiwa awe
ameshtakiwa kwa makosa aliyofanya kwenye mahakama ya wilaya ambayo kosa
limetendeka.
Ongolo alitakiwa kuomba dhamana Jumatatu lakini
mwanasheria anayemtetea, Lekoa Le-koko hakuwapo mahakamani, na hivyo
mashtaka kupangwa kusikilizwa tena jana.
Wakati mshtakiwa huyo akiwa mahakamani hapo
ulizuka mjadala mzito kati ya January na Mdu Thuketana ambaye alishika
nafasi ya Le-koko, wakijadiliana ni wapi mshtakiwa anaweza kushikiliwa
wakati kesi yake ikiendelea kusikilizwa.
Thuketana aliomba Ongolo awe chini ya ulinzi wa
polisi kutokana na afya yake kwani anasumbuliwa na maradhi ya pumu na
pia walikuwa wakihofia usalama wake.
Wiki iliyopita, Ongolo alishindwa kwenda mahakamani baada ya kuugua pumu na kupelekwa hospitali.
Hata hivyo, January alisema mshtakiwa anaweza
kuwekwa chini ya ulinzi wa polisi kwa siku saba tu, na baada ya hapo
atapelekwa kwenye mahabusu za kawaida, jambo ambalo liliafikiwa na
Hakimu Talijaard.
0 comments:
Chapisha Maoni