Ujenzi wa Soko la Mwanjelwa la jijini hapa ambao ulisimama kwa
karibu mwaka mzima unatarajiwa kuendelea tena mapema mwezi ujao kama
jiji litafanikiwa kupata mkopo mwingine kutoka Benki ya CRDB.
Mipango ya kupata mkopo wa Sh3.48 bilioni kuamuliwa Januari 23, mwaka huu
Meya wa Jiji la Mbeya, Athanas Kapunga aliwaambia
waandishi wa habari kwamba ujenzi huo utaanza kwa kumtumia mkandarasi
mpya wa ujenzi anayeitwa Nandhra Engineering and Construction Company
Limited ambaye atafanya kazi hiyo kwa gharama ya Sh5.3 bilioni.
Kapunga alisema kazi hiyo itatarajiwa kukamilika
chini ya miezi minane na kwamba mkandarasi huyo ametoa uhakikisho wa
kukamilisha kazi hiyo ikiwa mambo yatakwenda kama ilivyopangwa.
Hata hivyo, Kapunga alisema kuanza kwa kazi hiyo
kutategemea kukamilika kwa mipango ya kutaka kukopa zaidi ya Sh3.48
bilioni kwenye Benki ya CRDB ambayo bodi yake itakaa Januari 23 baada ya
jiji kuwasilisha nyaraka zote muhimu kwenye benki hiyo.
Akizungumzia utata na kukwama kwa ujenzi wa soko
hilo ambao ulianza Februari 25, 2010, Kapunga alisema mkandarasi mjenzi
Tanzania Building Works Company Limited alikwama kukamilisha ujenzi na
aliamua kuondoka eneo la ujenzi kutokana na matatizo anayoyajua yeye.
Alisema ujenzi huo ulikuwa ukifanywa kwa gharama
ya Sh 13 biloni ambazo zilikopwa Benki ya CRDB na ulitarajiwa kumalizika
Agosti 25,2011.
“Ujenzi hadi ulipofikia uligharimu zaidi ya Sh10.2
bilioni na salio la fedha zilikuwa Sh1.81 bilioni, lakini kwa bahati
mbaya riba nayo imekuwa Sh1.56 bilioni’’ alisema.
Kapunga alisema pamoja na utata huo, Benki ya CRDB
imeonyesha nia ya kutaka kutoa mkopo mwingine ili umalizie kazi hiyo
wakati Jiji nalo linalipa madeni pamoja na riba katika kipindi maalumu.
0 comments:
Chapisha Maoni