Sitta alisema anakubaliana na mawazo ya tume ya Warioba ya kuwa na
serikali tatu, lakini hakubali Rais wa Zanzibar na Tanganyika nao waitwe
marais, kama yule wa Muungano.
Akizungumza mjini Dar es Salaam jana, Sitta alisema ili serikali tatu
zifanye kazi kwa kuheshimiana, kuwekeana mipaka, rais wa Tanganyika na
wa Zanzibar, wapewe majina na hadhi nyingine, ili Tanzania iwe na rais
mmoja tu wa Muungano.
“Niliposikia maoni na ufafanuzi wa kina jinsi serikali tatu
zitakavyokuwa, nimekubaliana na mawazo ya tume kwamba tuwe na serikali
tatu. Lakini kwa maoni yangu tuwe na Amiri Jeshi Mkuu mmoja tu ambaye ni
Rais wa Muungano, maana hatuwezi kuwa na marais watatu kwenye nchi
mmoja,” alisisitiza Sitta.
Waziri huyo mwandamizi wa Serikali ya Rais Kikwete, alitoa mfano wa
Shirikisho la Afrika Mashariki (EAC) kwamba rasimu yake imependekeza
kuwa na rais mmoja tu na si marais sita, wanaounda shirikisho hilo.
Pia, alipendekeza jina la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
libadilishwe na badala yake, liitwe Shirikisho la nchi za Tanzania.
Akizungumzia msimamo wa Chama chake Cha Mapinduzi (CCM), kupinga
serikali tatu na kutaka muundo wa serikali mbili uendelee, Sitta
alisema: “CCM isibaki kuwa kichwa ngumu kupinga serikali tatu,”.
Alisema CCM inakosea kung’ang’ania serikali mbili wakati Katiba ya
Zanzibar ndiyo iliamua serikali mbili, hivyo serikali ya tatu kwa sasa,
haiepukiki.
Akitoa mfano, alisema Katiba ya Zanzibar inataka miswaada yote
inayopitishwa na Bunge la Jamhuri iridhiwe kwanza na Baraza la
Wawakilishi, jambo ambalo alisema si sahihi.
Alisema Katiba ya Zanzibar, imefanya mambo mengi kuihalalisha
Zanzibar kuwa nchi kamili na imefanya mambo hayo bila ridhaa ya Tanzania
Bara.
Alisema ili kubaki na serikali mbili, lazima Zanzibar ikubali
kuifumua Katiba yake inayotoa mamlaka kamili kwa rais wa visiwa hivyo,
jambo ambalo alisema ‘Wazanzibari hawawezi kulikubali’:
“Mimi nilipomsikiliza Jaji Warioba safari hii, jinsi alivyojenga hoja
ya serikali tatu, nimeona kuna hoja za msingi sana zipo kwa sababu kuna
mambo makubwa na ya msingi yameshafanyika,” alisema na kuongeza:
“Huwezi kupitisha Katiba inayosema miswada inayopitishwa bungeni
isifanye kazi Zanzibar hadi Baraza la Wawakilishi likae na kuridhia,
ukishafika hapo, basi serikali tatu haziepukiki,” alisisitiza Sitta.
Sitta alisema tume ya Warioba, imefanya kazi kubwa na nzuri kwani
rasimu ya pili imekwenda mbali kuangalia vitu kama zawadi za viongozi,
jambo ambalo zamani viongozi waliona ni haki yao kupata zawadi za aina
hiyo bila kujali kwamba hiyo ni rushwa.
Kwa mujibu wa Sitta – Kuna mambo ya msingi ya kuendelea kujadili nje
na ndani ya CCM, nayo ni namna ya kuiendesha Serikali ya Muungano, kwani
kwa maoni ya tume, serikali hiyo itakuwa ikichangiwa zaidi na
Tanganyika, jambo ambalo linaweza kuibua manung’uniko ya upande mmoja wa
Muungano.
Aliwataka Wana CCM na wadau wengine kuifanyia kazi kauli ya Rais
Kikwete aliyokaririwa mara kuwa vyama visipojali masilahi ya taifa
katika mchakato wa Katiba, – Katiba mpya itakwama na Watanzania
watalazimika kuendelea kutumia katiba ya sasa.



0 comments:
Chapisha Maoni