Kocha wa Yanga, Mholanzi Hans van der
Pluijm amesema uzoefu wake wa miaka 15 kufundisha soka barani Afrika
utasaidia kuipa mafanikio Yanga katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika
yanayoanza mapema mwezi ujao.
Akizungumza na Fichuo kwa njia ya mtandao akiwa Uturuki jana
, Kaimu
Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto alisema kocha huyo alibainisha
hayo mara tu baada ya mazoezi ya jana asubuhi.
“Nina uzoefu na soka la Afrika kwa takribani miaka 15, wachezaji
niliowakuta hapa (Yanga) wote wana uwezo mzuri, wanajituma, wana nidhamu
na upendo wa hali ya juu, mwalimu yoyote lazima atafurahia kwa kuwa
mazingira ya ufanyaji kazi yanakuwa mazuri,” alisema Kizuguto akimnuku
kocha huyo.
Kizuguto alisema Kikosi cha Yanga, ambacho kimepata pigo baada ya
kuzuiwa kwa usajili wa mshambuliaji wake hatari Mganda Emmanuel Okwi,
kiliendelea na mazoezi ya mwisho jana jioni na leo mchana kuanza kwa
safari ya kurejea Tanzania.
Aidha, ofisa huyo alisema kuwa Pluijm amesema kambi yao ya wiki mbili
kwenye mji unaotajwa kuwa wa matanuzi wa Antalya, Uturuki imekuwa na
manufaa makubwa katika kuimarisha kikosi na anaamini timu yake ipo
tayari kutetea ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom na kufanya vizuri
kimataifa.
“Hakuna majeruhi na wachezaji wanajituma na kuwajibika kwa kujua
wajibu wao. Tunashukuru Mungu kambi yetu ya siku 14 katika Hoteli ya
Sueno Beach Side, Manavgat jijini Antalya inakwenda vizuri,” alisema
Kizuguto.
Yanga ilikuwa imeweka kambi nchini Uturuki kwa wiki mbili kama
ilivyofanya mwaka jana, ikicheza michezo minne ya kirafiki dhidi ya timu
za Ankara Sekerspor (ilishinda 3-0) na Altay SK (ilishinda 2-0) za Ligi
Daraja la pili nchini humo kabla ya kuivaa timu ya KS Flumartari ya
Albania (0-0) kisha kumaliza na timu ya Simurq PIK ya Azerbajain (2-2).
Vinara hao wa msimamo wa Ligi Kuu Bara watacheza mchezo wao wa kwanza
mzunguko wa pili dhidi ya Ashanti United kwenye Uwanja wa Taifa jijini
Dar es Salaam keshokutwa.
0 comments:
Chapisha Maoni