Jumuiya ya Wafanyakazi wa Migodi na Ujenzi Afrika Kusini leo imeanza mgomo mkubwa katika sekta ya madini ya platinamu na hivyo kusimamisha shughuli katika migodi ambayo inazalisha nusu ya platinamu duniani.
Wafanyakazi wameanza mgomo katika migodi ya Anglo American Platinum, Impala Platinum and Lonmin na hivyo kusitisha uzalishaji wa platinamu ambayo ni muhimu katika vipuri vya magari. Msemaji wa Jumuiya ya Wafanyakazi wa Migodi na Ujenzi Jimmy Gama amesema mgomo huo umesitisha oparesheni zote katika migodi. Jumuiya hiyo ina wanachama 100,000 wanaofanya kazi katika ‘ukanda wa platinamu’ yapata kilomita 120 kutoka Johannesburg. Wafanyakazi waliogoma wanataka nyongeza maradufu ya mshahara wa awali huku wenye migodi wakisema watatoa nyongeza ya asilimia 7.5 hadi 8.5. Ikumbukwe kuwa mwaka 2012 kulikuwa na migomo katika migodi hiyo ambapo makumi ya watu waliuawa.
Inaelezwa kuwa, aghlabu ya mashirika katika sekta ya madini nchini Afrika Kusini yanamilikiwa na Wamagharibi ambayo licha ya kupata faida kubwa sana katika uwanja huo lakini yamekuwa yakiwalipa mishahara duni wafanyakazi wao.
0 comments:
Chapisha Maoni