Mbunge wa Viti Maalumu wa Chadema wa Mkoa wa Manyara, Paulina
Gekul jana alilazimika kuokolewa na polisi wilayani hapa, kutokana na
kushambuliwa na Mkurugenzi wa Halmashari ya Mji wa Babati, Omari
Mkombole na Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Mohamedi Fara, wakigombea
kabrasha lenye majina ya wanaopaswa kupewa ardhi.
Katika tukio hilo, Gekul ameeleza kuchaniwa nguo
zake, kudhalilishwa na kuporwa fedha zaidi ya Sh5 milioni zilizokuwa
kwenye mkoba wake.
Tukio hilo la kushambuliwa kwa mbunge huyo
lilitokea juzi saa 12 jioni katika ukumbi wa halmashauri ya mji wa
Babati, mara baada ya kikao kilichokuwa kikifanyika chini ya mkurungenzi
huyo kumalizika.
Akizungumza mara baada ya kutoka polisi jana kutoa
maelezo juu ya vurugu hizo, Gekul alisema kikao hicho kilichosababisha
vurugu hizo, kilikuwa kinajadili mustakabali wa ugawaji wa shamba la
Sisal Plantation lenye ekari 4200.
Alisema shamba hilo wakulima walilipia mwaka 2000
na Baraza la Madiwani lilikwishatoa uamuzi wa kugawanywa, lakini juzi
katika orodha iliyotolewa, alibaini majina mengi yameghushiwa na
walengwa wengi hawapo na baada ya viongozi wa halmashauri kubaini
amegundua njama hizo, ndipo waliagiza kurejeshwa makabrasha yote.
“Mimi nilikataa kwa sababu orodha hii ina makosa
na mimi nawafahamu baadhi ya wakulima wanaopaswa kupewa eneo hili
“alisema Gekul.
baada ya yeye kukataa kurejesha, aliahirisha kikao
na walipotaka kutoka nje ghafla alitokea Mkurugenzi wa halmashauri
hiyo, Omari Mkombole ambaye alidai alikwenda Polisi kufuatilia suala la
wakulima hao na tayari wanataka kuendesha msako wa waliovamia eneo hilo
bila idhini ya halmashauri.
“Lakini cha ajabu baada ya kusema hivyo,
mkurugenzi huyu akanifuata na kunikaba kwa nguvu, kisha kunichania nguo
zangu na kunipokonya karatasi akidhani zina majina ya wakulima hao,
Alisema baada ya mlango kufungwa alianza
kupokonywa kwa nguvu pochi yake na wakachambua ndani na kuondoka na
nyaraka zote, huku ufunguo wa gari ukitupwa.
Mkurugenzi wa Halmashauri Omari Mkombole,
alipopigiwa simu ya mkononi ili kuzungumzia tukio hilo, hakupokea na
simu yake iliita bila kupokewa, huku Mwenyekiti wa Halmashauri akikiri
kutokea kwa vurugu hizo.
0 comments:
Chapisha Maoni