Mawaziri saba na manaibu mawaziri 11 walikula kiapo mbele ya
Rais Kikwete, huku wengine watatu ikielezwa kuwa wataapishwa siku
nyingine kutokana na kutokuwapo nchini.
Mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yalifanyika juzi
ambapo mawaziri watano walitupwa na kuingizwa 10 wapya, kupandishwa
manaibu wanne kuwa mawaziri kamili na kuwahamisha wengine wanane kutoka
wizara zao kwenda nyingine.
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alisema
atafanya kazi kwa jitihada kubwa, uadilifu, ushirikiano na kutoa huduma
kwa wakati.
Nchemba ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM
alisema, “Nitafanya kazi kwa jitihada za hali ya juu, uadilifu,
ushirikiano na kutoa huduma kwa wakati. Watu wanadhani kuingia Wizara ya
Fedha ni kuchota fedha, binafsi nakwenda kusimamia sera”
Alisema moja ya mambo atakayohakikisha kuwa
anamshauri Rais Kikwete ni pamoja na kuhakikisha kuwa nchi inaachana na
utaratibu wa kuwa na bajeti tegemezi.
“Kuongeza vyanzo vya mapato kutakuja kama ukusanyaji wa kodi unasimamiwa ipasavyo na kupunguza matumizi ya Serikali,” alisema.
Alisema jambo jingine atakalolifanya ni kumshauri
Rais kuhusu Sheria ya Ununuzi lengo likiwa ni kuondokana na ununuzi wa
vitu mbalimbali kwa mtindo wa zabuni, kwa maelezo kuwa mtindo huo
huifanya Serikali kutumia kiasi kikubwa cha fedha.
“Jambo hili la ununuzi ni pana na linahitaji
kushauriana na kufanya uchambuzi wa kitaalamu. Pia nitashirikiana na
wenzangu kuhusu kuminya mianya mingine inayochangia Serikali kukosa
mapato yake ikiwa ni pamoja na kushirikiana na Ofisi ya Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),” alisema Nchemba.
Kwa upande wake, Waziri wa Katiba na Sheria, Asha
Rose Migiro alisema moja ya majukumu atakayoyafanya ni kuhakikisha kuwa
mchakato wa Katiba Mpya unakwenda kama ulivyopangwa, huku akisisitiza
kuwa hawezi kukipendelea CCM katika mchakato huo.
“Nitasimamia mchakato wa Katiba katika kipindi
hiki ambacho tunaelekea kwenye Bunge la Katiba na baadaye Kura ya Maoni.
Jambo zuri ni kwamba mchakato huu unakwenda kwa mujibu wa sheria.
Nawahakikishia Watanzania nitafanya kazi kwa uaminifu na kujituma,”
alisema Migiro.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufunzi,
Jenister Mhagama alisema sekta ya elimu kwa muda mrefu imekuwa na
changamoto nyingi na kwamba moja ya mambo atakayoyafanya ni kuhakikisha
kuwa anapambana na changamoto hizo.
0 comments:
Chapisha Maoni