Mahakama ya Mwanzo mjini Sumbawanga mkoani Rukwa jana iligeuka
uwanja wa mapambano kati ya Polisi wa Kituo Kikuu na familia ya Mzee
Anastazio Sikombe (62) baada ya familia hiyo kuanza kuwashambulia polisi
waliokuwa wakitaka kuwakamatwa kwa tuhuma za kuingia na kulima katika
shamba la mtu mwingine kinyume na sheria.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana na
kuthibitishwa na Polisi Mkoa wa Rukwa, tukio hilo lilitokea saa nne
asubuhi ikiwa ni muda mfupi tangu mzee huyo akiwa na familia yake ya
watoto watano wawasili katika viwanja vya mahakama hiyo kwa ajili ya
kufuatilia mwenendo wa shauri jingine ndipo polisi mmoja alipotaka
kuwakamata kwa madai walilima kwenye shamba la Ernest Mwanisenga (49)
kinyume na sheria.
Taarifa zinaeleza kuwa polisi huyo alipojaribu
kuwatia nguvuni familia hiyo ikiongozwa na mzee huyo walianza kumshushia
kipigo polisi huyo, lakini ghafla polisi wengine wapatao sita
walijitokeza na kuanza kumsaidia mwenzao kwa kupambana na familia hiyo,
sakata ambalo lilidumu kwa zaidi ya dakika saba hadi kumi na kuwafanya
watu kutoka katika vyumba vya mahakama ambako mashauri yalikuwa
yakiendelea na kwenda kushangaa tukio hilo.
Baadhi ya watu walioshuhudia tukio hilo walisema
kuwa mapambano hayo kati ya familia hiyo na polisi yalikuwa makali kwani
wanafamilia hao walikuwa wakijihami kwa kutumia silaha za jadi kama
fimbo na marungu, lakini walidhibitiwa na polisi hao kiasi cha mwenzao
mmoja kuzimia kwa dakika kadhaa ambapo muda mfupi baadaye gari yao aina
ya Defender lilifika na kuwachukua watuhumiwa hao na kuwafikisha kituo
cha polisi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda,
familia ya Mzee Sikombe ilikuwa na mgogoro mkubwa wa ardhi wakigombea
shamba lenye ukubwa wa ekari 40 katika Kijiji cha Tamasenga ambapo
mwishoni mwa mwaka 2013 Ernest Mwanisenga alifika Kituo cha Polisi
Sumbawanga na kufungua kesi ya kuingia kwa jinai namba 5202 ya ya mwaka
2013 akiwatuhumu mzee huyo na watoto wake kuingia na kulima kwenye
shamba lake kinyume cha sheria.
0 comments:
Chapisha Maoni