Mkuu Mpya wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali, Ernest Mangu
ameanza kazi kwa kutangaza mabadiliko ya mfumo wa jeshi hilo huku
akiunda vitengo vipya kwa lengo kuongeza ufanisi katika kukabiliana na
uhalifu.
Katika mabadiliko hayo, IGP Mangu amesema polisi
wameanzisha kamisheni mpya tano ambazo ni Intelijensia, Utawala, Fedha
na Ugavi, Upelelezi, Uchunguzi wa Kisayansi wa Kesi za Jinai na Polisi
Jamii.
Mfumo huo mpya wa polisi ndiyo uliowezesha kuundwa
kwa nafasi mpya ya Naibu IGP, ambayo mteule wake wa kwanza ni
Abdulrahman Kaniki ambaye kabla ya hapo alikuwa Kamishna wa Uchunguzi wa
Sayansi wa Makosa ya Jinai. Nafasi hiyo sasa inakaimiwa na watu
waliokuwa chini yake.
Viongozi wengine katika safu hiyo ni Mkurugenzi wa
Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Issaya Mngulu, Kamishna wa Operesheni
na Mafunzo, Paul Chagonja, Kamishna wa Fedha na Ugavi, Clodwig Mtweve,
Kamishna wa Utawala, Thobiasi Andengenye na Kamishna wa Polisi Jamii,
Mussa Ali Mussa. Naibu Kamishna wa Polisi, Diwani Athuman yeye anakaimu
nafasi ya Kamisheni ya Intelijensia.
Mabadiliko hayo yamekuja wakati Tanzania
ikikabiliwa na matukio ya uhalifu ambayo bado hayajapatiwa ufumbuzi wa
kiupelelezi, yakiwamo utekaji na utesaji wa watu, ulipuaji mabomu, watu
kumwagiwa tindikali, wizi kwa njia ya mitandao na mapigano kati ya
wakulima na wafugaji.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mangu
alisema amechukua hatua hiyo kutokana na changamoto ya kukabiliana na
aina mpya ya uhalifu ambao umekuwa ukijitokeza katika siku za karibuni.
Alifafanua kuwa zamani kazi za Fedha na Ugavi zilikuwa zikifanywa na kitengo cha Utawala na Utumishi.
Mangu alieleza pia kuwa Kamisheni ya Uchunguzi wa Kisayansi ni kitengo kipya katika jeshi hilo.
Alisema mabadiliko hayo yamelenga kuliwezesha jeshi hilo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi katika mazingira ya sasa.
“Jeshi limepanuliwa kidogo ili kukabiliana na
changamoto zilizopo na uteuzi huu ambao pia umefanya kuwapo kwa Naibu
IGP kwa mara ya kwanza una maana ya kuongeza ufanisi,” alisema Mangu,
akirejea hatua ya Rais Jakaya Kikwete kumteua Abdulrahman Kaniki
kushikilia nafasi hiyo mpya.
Alieleza kuwa wamepewa dhamana ya kuliongoza jeshi
hilo kutoka kwa mtangulizi wao, IGP Said Mwema huku kiwango cha uhalifu
kikiwa cha wastani na kuahidi kuupunguza maradufu.
Alisema wamepokea jeshi hilo tofauti na Mwema, ambaye alipopewa wadhifa huo 2006 kulikuwa na kiwango kikubwa cha uhalifu nchini.
0 comments:
Chapisha Maoni