Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), imesema Daftari la Kudumu la
Wapigakura, litafanyiwa marekebisho kabla ya kuanza kwa upigaji wa kura
ya maoni kwa ajili ya kupata Katiba Mpya, ili kuwawezesha vijana
waliotimiza umri wa miaka 18, ambao hawakujiandikisha, kupata fursa ya
kupigakura.
Imesema ili mtu aweze kupiga kura, lazima awe na
kitambulisho cha kupigia kura na si kitambulisho cha utaifa, kauli
ambayo inapingana na ile iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete kwamba
vitambulisho vya taifa vitatumika katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Hata hivyo kauli hiyo imekuja ikiwa imebaki miezi mitano kabla ya kuanza kwa upigaji wa kura ya maoni.
Upigaji wa kura ya maoni utafanyika ndani ya siku
74, ikiwa ni baada ya kumalizika kwa Bunge Maalumu la Katiba ambalo
litafanyika kwa siku 90, kuanzia Februari mwaka huu.
Jaji Lubuva alisema Nec itaendesha zoezi hilo kwa
kutumia mashine maalumu za kielekroniki na kusisitiza kuwa hawezi
kueleza tarehe rasmi kwa kuwa tume bado haijapata fedha kutoka
serikalini.
Alisema uboreshaji huo utaanzia ngazi ya vijiji ili kuondoa kero ya watu wanaokosa majina yao katika vituo vya kupigia kura.
“Nec ipo katika mchakato wa kuboresha Daftari la
Wapigakura kwa kutumia teknolojia ya kisasa, mfumo utakaotumika ni kama
ule unaotumiwa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA)” alisema Jaji
Lubuva.
Viongozi hao walipendekeza vitambulisho vya taifa
vitumike katika upigaji wa kura, ombi ambalo lilipingwa na Nec kwa
maelezo kuwa vitambulisho hivyo haviwezi kuwa mbadala wa vitambulisho
vya kupigakura.
Katika maelezo yake, Jaji Lubuva alisema Februari 9
mwaka huu, utafanyika uchaguzi wa udiwani katika Kata 27 Tanzania Bara
na kwamba katika uchaguzi huo daftari la wapigakura litakalotumika ni
lile lililotumika katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
“Kutokana na hali halisi hatuwezi kufanya
mabadiliko katika daftari la wapigakura ili tuwahi tarehe ya uchaguzi wa
udiwani katika kata hizi, lakini katika upigaji wa kura ya maoni pamoja
na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, daftari litakuwa limeboreshwa,”
alisema.
Hoja ya kutaka kuboreshwa kwa daftari hilo
ilitawala katika mkutano huo ambapo Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi
(CUF), Profesa Ibrahim Lipumba na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbroad
Slaa, waliowaongoza viongozi wengine kumbana Lubuva, ambaye alikiri wazi
kuwa suala hilo limekuwa kikwazo kwa wananchi.
0 comments:
Chapisha Maoni