Wizara ya Mambo ya Nje ya
Syria imeandika barua kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na kwa Rais wa
Baraza la Usalama la umoja huo ikiwataka wachukue hatua za kukabiliana
na uungaji mkono na utoaji misaada unaofanywa na Saudi Arabia kwa
makundi ya takfiri na ya kigaidi nchini humo. Katika barua hizo
imeelezwa kuwa kauli ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia kwamba nchi
yake inajivunia na kuona fahari kuwa inatuma silaha na kupeleka magaidi
huko Syria ni jambo la hatari na kwamba kuna ulazima wa kuchukuliwa
hatua kali dhidi ya serikali ya Riyadh.
Serikali ya Syria imeshaandika
barua kadhaa kwa jumuiya za kimataifa kuhusiana na harakati chafu
zinazoendeshwa na madola ya kigeni ndani ya nchi hiyo lakini hadi sasa
haijapata jibu lolote la maana. Hivi sasa pia ambapo Lakhdhar Brahimi,
mjumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu
katika mgogoro wa Syria yuko katika hekaheka za kukamilisha maandalizi
ya mkutano wa Geneva 2 ambao ajenda yake kuu ni kuutafutia ufumbuzi wa
kisiasa mgogoro huo, baadhi ya nchi kama Saudi Arabia zingali
zinaendelea kufanya uafriti ili kukwamisha juhudi hizo na wakati huohuo
kukoleza moto wa mgogoro nchini Syria.
Kuna ushahidi na nyaraka
chungu nzima zinazoonyesha kuwa serikali ya Saudia imekuwa ikiwaachia
huru wafungwa sugu walioko kwenye jela za nchi hiyo na kuwapeleka huko
Syria kupigana vita dhidi ya serikali ya nchi hiyo. Hatua kama hiyo
inaweza kuwa na maana nyengine ghairi ya kupalilia mbegu za fitina na
kukoleza moto wa mgogoro nchini Syria?
Kwa muda wote huu, msimamo wa
utawala wa kifalme wa Aal Saud kuhusiana na mgogoro wa Syria umekuwa ni
wa kuyasaidia kwa hali na mali makundi ya kigaidi yanayofanya hujuma
ndani ya ardhi ya nchi hiyo. Baadhi ya viongozi wa Syria wameutafsiri
msimamo huo wa Saudia kuwa ni sawa na kuuhalalisha kisheria ugaidi
nchini Syria na ambao ndio ukweli wa mambo. Katika kipindi cha miaka
mitatu iliyopita Saudi Arabia imekuwa mmoja wa wadhamini wakuu wa
misaada ya fedha na silaha kwa waasi na magaidi walioko nchini Syria, na
katika hili haiwezi kufumbiwa macho nafasi ya Bandar bin Sultan, mkuu
wa vyombo vya intelijinsia na vya usalama vya Saudia katika kuyaimarisha
magenge ya kigaidi nchini Syria. Aidha kuna taarifa nyingi
zinazoonyesha kuwa shirika la intelijinsia la Saudia, kwa kushirikiana
na baadhi ya nchi jirani na Syria ikiwemo Uturuki na Jordan, linawatuma
huko nchini Syria magaidi waliopewa mafunzo maalumu. Kwa msingi huo
hakuna shaka inayosalia kwamba kuibuka mgogoro nchini Syria na kuendelea
kwake ni matokeo ya mashirikiano ya waziwazi kati ya Marekani na
waitifaki wake wa eneo hususan Saudi Arabia, Qatar na Umoja wa Falme za
Kiarabu, Imarati.
Wizara ya Mambo ya Nje ya
Syria imetangaza kuwa asilimia 10 hadi 15 ya magaidi wanaofanya vitendo
vya ukatili na umwagaji damu nchini humo ni raia wa Saudi Arabia.
Magaidi hao wanaingizwa katika makundi kama vile Dola la Kiislamu la
Iraq na Sham, Harakati ya An Nusrah na magenge mengine ya kigaidi
likiwemo la Abdullah Azzam, ambayo yote hayo yanafuata miongozo ya moja
kwa moja au isiyo ya moja kwa moja kutoka kwa madola ya Magharibi na
Saudi Arabia. Nukta ya kuzingatiwa hapa ni kwamba makundi hayo ya
kigaidi yanatenda kila aina ya jinai nchini Syria bila ya hofu wala
kujali chochote. Kwa maelezo haya hakuna chembe ya shaka inayosalia
kwamba Syria imekuwa mhanga wa njama inayotekelezwa kwa ushirikiano wa
kambi mbili za Magharibi na ile ya Kiarabu, njama ambayo moto wake
utakuja kuzitambalia pia nchi za Kiarabu zinazofuata sera za Magharibi
na Marekani dhidi ya nchi hiyo



0 comments:
Chapisha Maoni