Bunge limeanza mchakato wa kutunga
Kanuni za Maadili na Mwenendo wa Wabunge ambazo zinalenga kuwabana, ikiwamo
hatua ya kuwapiga marufuku kuwa na nyaraka za siri zinazohusu utendaji wa
Serikali bila kibali cha mamlaka zinazohusika na utunzaji wa siri hizo.
Habari ambazo zimepatikana bungeni Dodoma
zinasema kanuni za maadili kwa wabunge ni matokeo ya kuwapo kwa tuhuma
mbalimbali zikiwamo za rushwa, ambazo zimekuwa zikielekezwa kwao, lakini Bunge
limekuwa likishindwa kuchukua hatua kutokana na kutokuwapo kwa kanuni husika.
Hata hivyo, tayari baadhi ya wabunge
wameonyesha kuzipinga kanuni hizo kwa maelezo kwamba zinalenga kuwanyima uhuru
wa kutekeleza majukumu yao kiufanisi.
Kanuni hizo ambazo ziko kwenye ngazi ya
rasimu,utunzi wake unaratibiwa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge
chini ya Mamlaka ya Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge inayolipa
mamlaka Bunge kuandaa kanuni za maadili kwa wabunge.
Kanuni za maadili zinazopendekezwa pia
zinatilia nguvu msingi wa utunzaji siri za Ofisi ya Bunge na nyaraka zote za
siri.
Rasimu ya kanuni hizo ambayo wanahabari
wameziona pia zinasema mbunge hatatumia taarifa atakazozipata kwa wadhifa wake
wakati akitekeleza shughuli za Bunge au Kamati ya Bunge kujinufaisha.




0 comments:
Chapisha Maoni