Wakati Serikali
ikisisitiza kuwa huduma ya kumwongezea mgonjwa damu hospitalini ni bure,
imebainika kwamba baadhi ya watu mitaani wakiwamo wabeba mizigo sokoni
wanauza damu zao kwa watu wanaohitaji.
Mbali ya watu kuuza damu zao, majimaji hayo
mekundu muhimu mwilini yamegeuka bidhaa adimu baada ya baadhi ya wauguzi
na madaktari nao kugeuza huduma hiyo kuwa kitegauchumi chao.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii,
ni kosa kwa mtumishi yeyote wa afya nchini kumuuzia mgonjwa damu na wala
hakuna biashara ya kuuza damu kwa kuwa hutolewa bure na watu
wanachangia kwa hiari.
Uchunguzi wa kina uliofanywa na gazeti hili katika
hospitali mbalimbali nchini, umebaini hospitali nyingi hazina damu za
kutosha na hivyo kusababisha baadhi ya wagonjwa kuwalipa watu mitaani,
ili kuwatolea damu au kuinunua kwa wauguzi na madakari.
Hata hivyo, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa
Jamii, Dk Seif Rashid alisema kuwa wahudumu wa afya wanaoendesha vitendo
hivyo ni watu wanaojaribu kuizidi maarifa Serikali na kwamba wananchi
wamepewa taarifa za kutosha kuwa damu haiuzwi.
“Kuna watu wanajaribu kutuzidi maarifa, hiyo ni
tabia inayopaswa kupigwa vita. Mtu yeyote atakayetakiwa kununua damu,
atoe taarifa kwa mganga mkuu au kituo chochote cha polisi,” alisema.



0 comments:
Chapisha Maoni