Bunge limefanya
mabadiliko makubwa katika kalenda ya mikutano yake ili kutoa fursa kwa
Bunge Maalumu la Katiba lililopangwa kufanyika kati ya Januari na Machi
2014.
Kamati ya Uongozi ya Bunge iliyokutana Jumatano
wiki hii chini ya uongozi wa Spika Anne Makinda ilifanya mabadiliko ya
mkutano wa 14 ambao sasa utaanza Desemba 3 na kuendelea kwa wiki tatu
hadi Desemba 20,mwaka huu.
Katika kalenda ya kawaida, mkutano huo ulipaswa kufanyika Februari mwakani.
Jana Makinda wakati akiongoza Bunge lililoketi
kama kamati kupitia muswada wa marekebisho ya sheria mbalimbali wa 2013,
alithibisha baadhi ya marekebisho katika sheria inayogusa mgawanyo wa
fedha katika Mfuko wa Elimu (TEA),yatafanywa katika mkutano wa 14
utakaofanyika mwezi ujao.
“Nadhani tukubaliane na maelezo ya Serikali
yaliyotolewa na Mwanasheria Mkuu,tunaweza kuangalia kipengele hicho cha
mgawanyo wa hesabu maana tunakutana tena hapa tarehe 3 ya mwezi
ujao,”alisema Makinda.
Habari ambazo zimeufikia mtandao wa Fichuo Tz zinasema
baada ya Bunge kuahirishwa jana, wabunge watakuwa na wiki moja tu ya
mapumziko hadi Novemba 17, watakaposafiri kwenda Dar es Salaam kwa ajili
ya kuanza vikao vya kamati Novemba 18.
Mkutano huo wa 14 pamoja na mambo mengine
unatarajiwa kujadili Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG), ripoti za mwaka za utendaji za Kamati za Kudumu za Bunge
pamoja na kushughulikia miswada ambayo haikuweza kupitishwa katika
mikutano ya 12 na 13.
Mabadiliko hayo pia yanalenga kuwezesha Bunge
Maalumu la Katiba kufanyika na kuhitimisha kazi yake ifikapo Machi mwaka
huu, ili kutoa fursa kwa maandalizi ya Bunge la Bajeti ambalo kwa
mujibu wa kalenda hufanyika kati ya Aprili na Julai.
Mpangilio huo wa shughuli mfululizo
zinazowahusisha wabunge umeanza kulalamikiwa na baadhi yao kwamba
utawaweka mbali na majimbo yao kwa muda mrefu, kuliko ilivyo kawaida.
Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu
na Bunge), William Lukuvi alikiri kuwapo kwa mabadiliko hayo,lakini
akasema taarifa rasmi inapaswa kutolewa na Ofisi ya Bunge.
Kabla ya kikao cha Kamati ya Uongozi,Katibu wa
Bunge,Dk Thomas Kashililah alikiri kuwapo kwa kusudio la kufanya
mabadiliko, lakini akasema zilikuwa zikisubiriwa baraka za kamati hiyo.
Mwanzoni mwa wiki hii,Spika Makinda aliwatangazia
wabunge kwamba wanakusudia kufanya mabadiliko kweye kalenda ya Bunge ili
kutoa mwanya wa kufanyika kwa Bunge Maalumu la Katiba, bila kuathiri
mikutano ya Bunge iliyopo kikatiba



0 comments:
Chapisha Maoni