Denis Mukwege, tabibu wa magonjwa ya wanawake raia wa Kongo ametunukiwa tuzo ya ushujaa ya kiraia ya mwaka 2013 kuenzi huduma za kibinadamu anazozitoa katika eneo lililoathiriwa na vita la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Dakta Mukwege amekuwa miongoni mwa wagombea waliopendekezwa kuwania tuzo ya amani ya Nobel kwa mwaka huu wa 2013.
Tabibu huyo wa magonjwa ya wanawake raia wa Kongo amepokea tuzo hiyo jana kutokana na huduma zake anazotoa katika hospitali ya Panzi, ambayo huwahudumia raia walioathiriwa na vitendo vya ubakaji huko mashariki mwa Kongo.
Umoja wa Mataifa umeeleza kuwa jeshi la Kongo na baadhi ya makundi yenye silaha ikiwemo harakati ya waasi ya M23 yamekuwa yakijihusisha na vitendo vya kuwabaka raia huko mashariki mwa Kongo.
Dakta Denis Mukwege amesema kuwa kitendo cha kuwahudumia wanawake hao wa mashariki mwa Kongo waliobakwa kimebadili maisha yake.
Amesema kazi yake ya udaktari imemfanya awe shuhuda wa moja kwa moja wa jinai kubwa ambayo ni vigumu kuielewa kikamilifu.



0 comments:
Chapisha Maoni