Jumanne, Septemba 17, 2013

MLOLONGO WA MAUAJI WAENDELEA MAREKANI, SASA NI KAYIKA JESHI LA MAJINI

Kwa mara nyingine tena jamii ya Marekani imeshuhudia ufyatulianaji risasi wa kiholela uliopelekea roho za watu kupotea. 
Watu 12 wameuliwa na mtu aliyekuwa na silaha aliyevamia kambi ya jeshi la majini mjini Washington. Aaron Alexis aliyewahi kuhudumu katika Jeshi la Majini la Marekani kwa muda wa miaka minne aliingia na silaha katika jengo la jeshi hilo huko Washington na kuanza kufyatua risasi ovyo kabla ya kupigwa risasi na kuuliwa na maafisa wa polisi waliokuwemo kwenye jengo hilo. 
Licha ya kupita masaa mengi tangu lilipotokea tukio hilo lakini bado sababu zilizomfanya afisa huyo wa kijeshi kufanya shambulizi hilo hazijajulikana. Kuna maneno mengi yanasemwa kuhusiana na sababu za shambulio hilo. 
Wengine wanasema huenda Alexis alipata kichaa na wendawazimu, wengine wanadai pengine alifanya hivyo ili kulipiza kisasi huku wengine wakisema yamkini Alexis alikuwa anapinga siasa za kijeshi za Marekani.
Hata hivyo tukiachana na sababu zilizompelekea afisa huyo wa kijeshi kubeba silaha na kuanza kuwafyatulia risasi ovyo maafisa wenzake, kuna jambo moja hapa haliwezi kupingika hata kidogo nalo ni kwamba hakuna sehemu yoyote nchini Marekani iliyo salama, hata katika majengo yenye ulinzi mkali ya jeshi la nchi hiyo.
Miaka michache iliyopita tukio kama hilo lililotokea katika kambi kubwa zaidi ya kijeshi ya Marekani mjini Texas wakati daktari mmoja wa saikolojia na matatizo ya akili wa jeshi la nchi hiyo alipoamua kubeba silaha na kwenda kuua wafanyakazi wenzake kadhaa.
Tab'an kwa vile daktari huyo alikuwa Muislamu, viongozi wa Marekani na vyombo vyao vya habari havikupata tabu kuliita tukio hilo kuwa la kigaidi.
Kwa kweli tukio hilo la Texas nalo lilithibitisha kwa mara nyingine kuwa jeshi la Marekani halikujitengenezea maadui wa nje tu, bali limejipalilia mkaa wa kuwa na maadui hata wa ndani yake lenyewe jeshi hilo.
Wakati wanajeshi 300 tu wa Marekani wakiwa ndio walioripotiwa kuuawa katika mapigano ya miaka 11 ya nchini Afghanistan, watu 20 wameuawa kiholela katika matukio mawili tu ya ufyatuaji risasi kwenye kambi mbili za kijeshi ndani ya Marekani.
Tab'ani mauaji ya kiholela katika mitaa ya miji ya Marekani ni makubwa zaidi kuliko ndani ya taasisi za kijeshi. Katika siku za mwishoni mwa mwaka uliopita, watu 25 waliuliwa wakiwemo watoto wadogo 20 wakati kijana mmoja alipovamia shule moja ya jimbo la Connecticut na kuitumbukiza jamii ya Marekani katika bumbuwazi na majonzi makubwa.
Kabla ya shambulio hilo, watu wengine 10 waliuliwa kwenye jumba moja la sinema katika jimbo la Colorado. Tukio jingine kama hilo lilitokea katika Chuo Kikuu cha Virginia na kukumbushia mauaji mengine makubwa ya kiholela yaliyotokea mwaka 1990 kwenye shule moja ya jimbo la Colorado.
Matokeo yote hayo yamedaiwa kufanywa na watu punguwani wa akili au waliokata tamaa katika maisha yao. Marekani ni nchi ambayo watu wanaruhusiwa kumiliki silaha wanavyopenda. Kati ya kila watu 10, tisa kati yao wanamiliki silaha moto.
Takwimu zinaonesha kuwa, zaidi ya matukio 20 elfu ya mauaji ya kiholela yanatokea nchini Marekani kila mwaka.
Vile vile sehemu kubwa ya wafungwa milioni mbili walioko katika jela za Marekani wamepatwa na hatia za kutumia vibaya silaha moto. Alaakullihaal, wahanga wakuu wa mlolongo huo usio na mwisho wa mauaji ya kiholela ni wananchi wa kawaida wa Marekani ambao hukumbwa na mauti ya ghafla wakiwa mashuleni, katika Vyuo Vikuu, kwenye majumba ya sinema, katika maduka, barabarani na hata ndani ya kambi za kijeshi.
Kwa kweli wananchi wa Marekani wanaishi katika mazingira ambayo hawajui ni wakati gani mtu fulani atarukwa na akili na kuanza kuwafyatulia risasi ovyo watu wasio na hatia.

0 comments:

Chapisha Maoni