Ijumaa, Septemba 06, 2013

HII NDIO SABABU YA MREMA KUTOSUSA MJADALA WAKATI WENZAKE WALIPOSUSIA JANA NA JUZI

Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP)Augustine Mrema amejitetea akisema si kibaraka au pandikizi la CCM baada ya kukataa kuungana na wapinzani wenzake kususia mjadala wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013 jana na juzi.
 
Akichangia mjadala huo, Mrema ambaye ni Mbunge wa Vunjo, alisema hakutoka nje kwa kuwa ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Demokrasia Tanzania (TCD) inayoundwa na vyama vyote vya siasa vyenye wabunge kikiwamo CCM.
Huku akishangiliwa na wabunge wa CCM, Mrema alijigamba kuwa yeye ni bosi wa vyama vyote ndiyo maana ilibidi abaki bungeni ili kuangalia kinachoendelea. Alisema kama angeamua kutoka kama walivyofanya wabunge wa Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi, basi ingekuwa sawa na kushindwa kusimamia majukumu yake ya TCD kikamilifu.
Mrema alikuwa akichangia hoja hiyo wakati wabunge vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi wakiwa wametoka.
Juzi usiku, Mrema alikuwa mbunge pekee wa upande wa upinzani aliyebaki ndani ya Ukumbi wa Bunge baada ya wabunge wengine kutoka wakipinga kujadiliwa kwa muswada huo bila ya kuwashirikisha kikamilifu wadau wa siasa kutoka Zanzibar.

0 comments:

Chapisha Maoni