Wakati Serikali leo ikitarajiwa kuirejesha Katiba ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa ajili ya kufanyiwa marekebisho, Mdau wa soka aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Tanzania (FAT), Michael Wambura ‘amechekelea’ uamuzi huo kupitia Msajili wa Vyama vya Michezo na Vilabu.
Katikati ya wiki hii, Waziri wa Michezo, Amosi Makala alipinga uamuzi wa Rais wa TFF, Leodegar Tenga kutangaza kamati kadhaa, akisema hatua hiyo ni batili kwa vile marekebisho ya Katiba ya TFF hayakuwa yamepitisha na Msajili.
Makala alisema kuwa, marekebisho ya katiba hiyo yana upungufu na kwamba, uamuzi wa Tenga kuunda kamati za TFF ni batili.
Katika taarifa yake aliyoisambaza kwa vyombo vya habari jana, Wambura alisema anaunga mkono uamuzi huo kwa vile utaratibu uliotumika kubadili katiba hiyo haukufuata taratibu zilizoainishwa kwenye Katiba ya TFF na sheria za nchi.
Alizitaja sababu sita zilizomfanya aunge mkono kukataliwa kwa marebebisho hayo, kuwa ni upigaji kura wa marekebisho ya katiba, mkutano mkuu wa dharura na uingizaji wa vifungu kwenye katiba bila ya kujadiliwa na kupitishwa na Mkutano Mkuu TFF.
Sababu nyingine ni uundwaji wa kamati kabla ya marekebisho ya katiba, ukomo wa madaraka wa viongozi wa vyama na kuwapo kwa hila za kuvuruga mchakato wa uchaguzi. Akizungumzia upigaji kura wa marekebisho ya katiba alisema, zoezi hilo ni batili kwa vile hakuna kura zilizopigwa na wajumbe wa Mkutano wa TFF na kuhesabiwa kuamua ama kupitisha au kukataa.
0 comments:
Chapisha Maoni